May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Gwajima asimamisha watano Ukerewe

Spread the love

WAZIRI wa Afya nchini Tanzania, Dk. Dorothy Gwajima, amewasimamisha watumishi watano wa Hospitali ya Wilaya ya Nansio Ukerewe jijini Mwanza, kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili. Anaripoti Danson Kaijage, Mwanza …(endelea).

Watumishi hao ni wale waliokuwa wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa dawa zenye thamani zaidi ya Sh.200 milioni ambapo mmoja wao alikiri na kuhukumiwa kulipa Sh.100 milioni na waliobakia walirejeshwa kazini.

Watumishi hao wamesimamishwa kazi kufuatia agizo la Dk. Gwajima alipofanya ziara katika Hospitali hiyo hivi karibuni.

Amesema, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cornel Magembe kuwa naye hakuridhishwa na watumishi hao kurejeshwa kazini kwani hawaaminiki tena kwenye utumishi wa umma na kamwe haieleweki inawezekanaje mtumishi wa umma aibe halafu akishalipa anarejeshwa kazini.

Mara baada ya Dk. Gwajima kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Nansio alijionea kuendelea kuwepo kwa viashiria vya udanganyifu katika mfumo mzima wa ugavi wa dawa hivyo kukubaliana na maelezo ya Mkuu wa Wilaya kuwa bado kuna tatizo kama alivyoeleza.

Hivyo, alimuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Ukerewe, Esther Chaula kuwasimamisha kazi watumishi hao na kuwafikisha kwenye kamati ya maadili ya utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma na vyama vyao ili waone kama kweli hao watumishi bado wanastahili kuaminika kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma pia maadili ya vyama vyao vya kitaaluma.

“Mahakama imefanya maamuzi kwa mujibu wa sheria wakalipa, hata hivyo naagiza Mkurugenzi kama tulivyokubaliana uendelee kusimamia hatua za kinidhamu na kiutumishi,” amesema Dk. Gwajima

Pia, amesema, uwafikishe kwenye mabaraza na bodi zao za taaluma pamoja na vyama vyao vya taaluma ili nao wawachunguze na kuwachukulia hatua.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk.Thomas Rutachunzibwa amesema, watumishi hao ambao ni wataalamu wa maabara, Famasi na Daktari wameshasimamishwa kazi huku hatua zaidi za kinidhamu, maadili na kiutumishi zikiendelea kuchukuliwa dhidi yao sambamba na uchunguzi wa mabaraza na bodi za kitaaluma.

error: Content is protected !!