Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Waziri Aweso azipa siku 30 mamlaka za maji, aipongeza Dawasa
Habari Mchanganyiko

Waziri Aweso azipa siku 30 mamlaka za maji, aipongeza Dawasa

Spread the love

 

WAZIRI wa Maji nchini Tanzania, ametoa siku 30 kwa mamlaka zote za maji, kufanya ukaguzi kwa wateja wote wanaowahudumia ili kupata takwimu sahihi ya wanaowahudumia na upotevu wa maji. Anaripoti Ibrahim Yamola, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, ameagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kuratibu mpango wa kubaini gharama halisi za kuwaunganishia maji wananchi ambazo zitaanza kutumika nchi nzima, kama ilivyo kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Waziri Aweso, amesema hayo leo Jumanne, tarehe 6 Julai 2021, katika mkutano wa kujitathimini walipotoka, walipo na wanapokwenda wa Dawasa, inayohudumia mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Katika shughuli hiyo, Waziri Aweso amezindua magari ya kukusanya majitaka na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh.4 bilioni. Pamoja na kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora, akiwemo Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Agizo hilo, amelitoa wakati akizungumzia suala la upotevu wa maji akidai, kuna maeneo amekuwa akitembelea na kuelezwa “upotevu wa maji ni asimilia 42” jambo ambalo hakubaliana nalo.

“Unaposema upotevu wa maji ni asilimia 42, ina maana kwamba nikienda huko kuangalia hali halisi nikute madimbwi ya maji na wizara ya uvuvi wanafuga samaki, lakini hali imekuwa tofauti,” amesema

Kutokana na hili, “tunatoa zoezi la mwezi mmoja, kwa mamlaka zote za maji, kukagua mteja kwa mteja anayempatia huduma ya maji, ili kudhibiti hawa mnaosema wanapoteza maji.”

Aidha, Waziri Aweso amesema, katika siku hizi 30, “kuwe na timu kupita katika maeneo yote kudhibiti upotevu wa maji.”

Kuhusu gharama za kuwaunganishia maji wananchi, Waziri Aweso amesema “bado siridhishwi na gharama za kuunganishiwa maji, kwa nini tunashindwa kujua ni bei gani? Niwaombe sana, mje na gharama halisi na Dawasa naomba mkalifanyie kazi.”

“Katika hili, lisiwe na ubabaishaji, mwananchi amelipia ili aunganishiwe, aunganishiwe haraka, hii kazi mnaiweza na nendeni mkaifanye, mje na bei halisi, kama Tenesco wameweza kuwa na gharama kwa nini sisi tushindwe,” amehoji Aweso

Katika mkutano huo, Aweso ameipongeza Dawasa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwasogezea wananchi huduma huku akizitaka mamlaka zingine za maji nchini, kwenda kujifunza Dawasa inavyofanya kazi.

Dawasa inayoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Cyprian Luhemeja na Mwenyekiti wa Bodi ya mamlaka hiyo, Jenerali mstaafu, Davis Mwamnyange, waziri huyo amesema, “nimpongeze sana mwenyekiti wetu wa bodi, Jenerali Mwamunyange, ndugu yangu Luhemeja kwa kazi kubwa mnayoifanya.”

“Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, CEO Luhemeja unafanya kazi kubwa sana na nikiwa waziri wa maji, naridhishwa sana na utendaji wako. Yaani naweza kusema Dawasa ni noma, noma nooooma sana,” amesema Aweso

Waziri huyo amesema, juzi alipigiwa simu na Jenerali Mwamnyange “ulinipigia simu kuomba upumzike kwa kazi kubwa uliyoifanya, lakini hapana. Nitamwomba na kumshauri Rais (Samia Suluhu Hassan), bodi ya Dawasa iendelee na bodi zingine za maji, zije kujifunza Dawasa ambacho ni kama chou.”

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange alisema, wataendelea kutekeleza miradi mkubwa na midogo kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa asilimia 100 kabla yam waka 2025.

Huku akishangiliwa, Jenerali Mwamnyange amesema “nawapenda sana wafanyakazi wa Dawasa. Naipenda Dawasa kutoka moyoni. Tangu nilipoteuliwa kuwa mwenyekiti nimeshuhudia uzalendo, ujasiri, ushirikiano kwa kweli ninyi ni bora.”

Jenerali huyo mstaafu amesema “ningeweza au natamani Dawasa lingekuwa na jina la pili vilevile kwamba Dawasa liitwe jina la pili Jeshi la Huduma ya Maji kwa Wananchi ya Dar es Salaam na Pwani.”

“Wananidhamu sana na CEO (Luhemeja) ningetamani awe na jina la pili, Mkuu wa Jeshi la Huduma ya Maji.

Akitoa maelezo ya upatikanaji wa maji, Mhandisi Luhemeja amesema, kwa sasa upatikanaji wa maji kwa maeneo wanayoyahudumia ni asilimia 92 “na malengo yetu ifikapo Juni 2023 tuwe tumefikia maeneo yote kwa asilimia 100.”

Amesema, kwa sehemu kubwa, wanatumia fedha za ndani kugharamia miradi mbalimbali mikubwa na midogo lengo ni kuhakikisha wanatekeleza kwa wakati ili kufikia malengo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!