July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri Aweso awaonya RUWASA, atoa maagizo

Waziri wa Maji, Juma Aweso

Spread the love

 

WAZIRI wa Maji nchini Tanzania, Jumaa Aweso amewataka Mameneja wa Wilaya na Mikoa wa Mamlaka za Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Aidha, amewataka miradi inatoa maji kama ilivyokusudiwa ili wananchi waweze kupata huduma hiyo muhimu na kuacha kuongea uongo kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji kwani mambo hayo yanarudisha nyuma utendaji na utekelezaji wa miradi ya maji.

Aweso ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kupokea ripoti ya taarifa ya utendaji wa RUWASA kwa mwaka fedha 2020/2021 na kutiliana saini mikataba ya dira za maji za malipo ya kabla ya kutumia zitakazowezesha kuondoa malalamiko miongoni mwa wananchi ya kubambikiziwa bili za maji.

“Huko nyuma kulikuwa na ubabaishaji katika utekelezaji wa miradi ya maji, unaenda sehemu kuangalia mradi, unakuta mradi hewa, lakini kabla hujafika eneo la tukio mtaalam anakwambia mradi umetekelezwa na wananchi wanapata maji,” amesema.

“Hatuwezi kukubali mambo hayo kuendelea lakini hatuwezi kukubali kukubali kuona mwananchi ananyanyasika kwa sababu ya maji na hatutaki kuona wananchi kunywa maji na punda kuwa kama ndio haki yao,” amesema Aweso

Amesema alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji mwaka 2017 kulikuwa na viongozi walikuwa wakiongea kuhusu miradi ya maji na hivyo kufanya nchi kuwa na miradi hewa ya maji na iliyoonekana ilikuwa haitoi maji.

Hata hivyo amesema baada ya kuundwa kwa RUWASA na kuwekana sawa na viongozi mambo yamebadilika ambapo hivi sasa miradi mingi inatoa maji na ambayo bado mpaka Desemba 2022 upo uwezekano mkubwa wa kuwa imeshakamilika.

“Wakati huo miradi chechefu ilikuwa 177, lakini baada ya kuanzishwa RUWASA miradi 126 kati ya hiyo imekwamuliwa bado kama miradi 51 ambayo naamini hadi kufikia Disemba itakuwa imekamilika,” amesema Aweso

Katika hafla hiyo ambayo pia kulikuwa na makabidhano ya pikipiki kwa Jumuiya za watumiaji maji na ofisi za mikoa za RUWASA, Aweso amesema mita za malipo kabla ya kutumia maji zitasaidia kuoa kero miongoni mwa wananchi za kubambikiziwa bili za maji huku akisema dunia ndiko inakopaswa kwenda kulingana na teknlojia inavyokua.

“Wenzetu Tanesco wapo vizuri, walishaachana na malalamiko ya wananchi ya kubambikiziwa bili kwa kuanza matumizi ya mita za malipo kabla ya matumizi,” amesema.

Bomba la maji

Pia amezitaka Jumuiya za Maji vijijini zenye tabia ya kugawana fedha za maji kuacha tabia hiyo mara moja ili kuifanya huduma ya maji katika maeneo kuwa endelevu.

Kuhusu pikipiki zilizotolewa amewataka wahusika watakazopewa pikipiki hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ya kufuatilia na kusimamia miradi ya maji na siyo kwa ajili ya matumizi ya bodaboda.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi aliwataka viongozi na watumishi wa RUWASA kwa ujumla kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kila mmoja atimize wajibu kikamilifu.

Awali, Mtendaji Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Clement Kivegalo alisema, RUWASA imetiliana saini na Chuo cha Ufundi Arusha, Dar es Salaam Teknohama Institute (DTBI) na Chuo Kikuu cha Mbeya (MUST) ambapo vyote kwa pamoja vinakwenda kutengeza mita za malipo kabla ya kutumia zipatazo 350.

Naye Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde alisema ofisi yake ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Maji kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kikamilifu.

error: Content is protected !!