December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri awafuta kazi walimu waliombadilishia namba ya mtihani mwanafunzi la 7

Spread the love

 

SERIKALI imeifungia Shule ya Awali na Msingi ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha Mitihani pamoja na kuwafuta kazi wasimamizi wa mtihani ambao ni walimu kutokana na udanganyifu uliofanyika katika Mtihani wa darasa la Saba uliofanyika tarehe 5,6 Oktoba, 2022.

Pia mmiliki wa shule hiyo binafsi ameagizwa kuwafuta kazi walimu waliohusika katika uzembe huo na asipotekeleza agizo hilo Kamishna wa elimu mkoa wa Pwani ameagizwa kuifutia usajili wa shule hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika uchunguzi wa taarifa zilizotolewa na mwanafunzi Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha Mtihani wa shule ya Awali na Msingi cha Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya mtihani wa somo la mwisho.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Oktoba, 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani na ule wa wataalamu wa miandiko “forensic” uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini ufanano wa miandiko kwa watahiniwa saba wa shule hiyo .

“Uchunguzi umebainika jumla ya watahiniwa saba walibadilishiwa namba za mtihani katika kituo cha mtihani namba PS1408009 shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic” amesema Profesa Mkenda.

Uchunguzi huo ulifanywa baada kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii ikimuonesha mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha mtihani cha shule ya Awali na Msingi Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba, alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) uliofanyika Oktoba 05 na 06/10/2022.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda

Amesema baada ya kupata taarifa hiyo Serikali kupitia Baraza la Mitihani ilielekeza Kamati ya Uendeshaji Mitihani ya Mkoa wa Pwani kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya mtahiniwa na kuwasilisha taarifa Baraza la Mitihani.

“Uchunguzi uliofanyika pia umebaini kuwa mwanafunzi huyo pamoja na wanafunzi wengine sita walibadilishiwa namba ya mtihani katika mtihani wa taifa wa darasala saba.

“Mtahiniwa Iptisam Suleiman Slim alifanya masomo matano kwa kutumia namba PS1408009/0040 na somo la sita (mwisho) kwa kutumia namba PS1408009/0039 na Watahiniwa wengine wanne pia walibadilishiwa namba katika somo la sita katika kituo hicho,” amesema.

Amesema kulikuwa na uzembe uliofanyika hivyo pamoja na kuifungia shule hiyo watumishi wa Serikali ambao walikuwa wasimamizi wa kituo hicho watachukuliwa hatua za kinidhamu ambazo si nyingine bali ni kufutwa kazi.

Amesema hatua hizo zinachukuliwa kwa kuwa hayo ni makosa ambayo yanaweza kumyima mtu haki yake ya kuendelea na elimu.

Amesema uzembe huo pia ulionekana dhahiri kwa sababu inawezekana walibadilisha namba kwa uzembe lakini baada ya wanafunzi kuongea walimu hao wakawaambia wanafunzi msiseme lakini cha ajab hawakutoa taarifa ya makosa yao.

“Wale ambao ni waajiriwa wa serikali nimeandika barua wachukuliwe hatua za kinidhamu na ninaamini watafukuzwa kazi, sidhani kama kuna adhabu zaidi ya kutosha kutuma ujumbe kwamba hatutaki kufanya uzembe kwenye mitihani zaidi ya kuwafukua kazi moja kwa moja,” amesema.

Aidha, kufuatia changamoto hiyo Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefanya marekebisho ya namba za Mtihani za watahiniwa husika ili kila mtahiniwa aweze kupata matokeo yake halali.

“Nakupongeza Mwanafunzi Iptisam kwa kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa, tayari NECTA imefanya marekebisho hata kwa wengine ambao wamefanyiwa udanganyifu kama huo. Natoa wito kwa wananchi na wanafunzi wote ukiona mtu anafanya mchezo kwenye mitihani toa taarifa na Serikali itachukua hatua mara moja,” ameongeza Prof. Mkenda.

Kwa upande wake mzazi wa mwanafunzi Iptisam, Suleiman Said ameishukuru Serikali kwa kufanyia kazi changamoto hiyo aliyoipata mtoto wake wakati wa kufanya mitihani yake ya kuhitimu darasa la Saba.

Pia amevishukuru vyombo vya Habari kwa kutoa taarifa hiyo na kuweza kuwafikia walengwa na kuifanyia kazi.

error: Content is protected !!