Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Waziri amvua madaraka mkuu idara ardhi
Habari Mchanganyiko

Waziri amvua madaraka mkuu idara ardhi

Angelina Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi
Spread the love

ANGELINA Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, amemvua madaraka mkuu wa idara ya ardhi wa Wilaya ya Ukerewe, Elia Mtakama, kwa kushindwa kuingiza viwanja katika mfumo wa ukusanyaji wa kodi pamoja na kushindwa kupima viwanja, anaandika Charles Mseti.

Mtakama pia anatuhumiwa kushindwa kuainisha idadi ya viwanja vilivyopimwa na kushindwa kupima taasisi za umma na kutoa hati za umiliki wa viwanja kitendo ambacho kinaendelea kusababisha migogoro ya ardhi wilayani humo.

Akizungumza na watumishi wa idara hiyo pamoja, wakuu wa idara mbalimbali pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo, Mabula alisema kuwa mkuu huyo wa idara hakuwa na sifa za kuongoza idara hiyo na badala alisababisha shughuli za upimaji na ukusanyaji kodi ya ardhi kusuasua.

Amesema kuwa licha ya Serikali kutoa agizo la kila halmashauri nchini kuhakikisha zinapima makazi holela pamoja na kutumia mfumo bora wa ukusanyaji wa kodi kwa kuingiza viwanja vyote vilivyopimwa na ambavyo havijapimwa kwenye mfumo huo, lakini wilaya hiyo haijatekeleza agizo hilo.

“Migogoro ni mingi sana kwenye wilaya yenu lakini ardhi yenu ni ndogo na ni kutokana na huyu mkuu wa idara (Elia Mtakama) kufanya kazi kwa mazoea, ameshindwa kusimamia idara yake na hafai kuendelea katika nafasi hii tena.

“Mkurugenzi (Frank Bahati) kuanzia sasa huyu si afisa ardhi tena, hatuwezi kuwa na mtu kama huyu na anakuja hapa anasoma taarifa kwa mbwembwe utafikiri taarifa ni nzuri sana… na tumieni mtu mwingine hata kutoka halmashauri nyingine ya jirani,” amesema Mabula.

Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela mkoani hapa, alisema kuwa taarifa hiyo ilikuwa na mapungufu mengi ikiwemo kutoonesha changamoto zinazokwamisha upimaji ardhi pamoja na kushindwa kuonesha lengo la ukusanyaji kodi pamoja na kutaja kiasi cha Sh. milioni 140 walizokusanya.

Pia Mabula ameiangiza wilaya hiyo, kumpelekea taarifa za taasisi za umma zinazodaiwa kodi ya ardhi na kuzipa notisi ya siku 14 kulipa fedha wanazodaiwa na kwamba kama hazitatekeleza notisi hiyo zifikishwe kwenye baraza la ardhi ili zisurutishwe kulipa kwa lazima.

Estomiah Chang’ah, Mkuu wa Wilaya hiyo na yeye alipigilia msumali kwenye kauli ya Mabula na kusema, “Mimi mwenye niliwauliza kuhusu ukusanyaji wa kodi kwa kutumia huo mfumo wakaniambia mfumo haufanyi kazi kwa sababu ya mtandao wanaotumia sio mzuri,” alisema Chang’ah.

Kwa upande wake mkuu huyo wa idara, Elia Mtakama, alisema kuwa sababu zilizochangia washindwe kupima viwanja wilayani humo ilichangiwa na migogoro ya ardhi iliopo baina ya halmashauri hiyo na wananchi.

Naibu waziri huyo, amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoa wa Mwanza ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na watumishi wa idara ya ardhi na kuzungumza nao kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kazi na kukagua mfumo mpya wa ukusanyaji kodi ya ardhi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!