August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri alidai Mseto fidia Bil. 1

Spread the love

EDWIN Ngonyani, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amelitaka gazeti la Mseto kumuomba radhi pia kumlipa fidia ya Sh. 1 bilioni kwa madai ya kuandika habari za uongo dhidi yake, anaandika Regina Mkonde.

Gazeti la Mseto linachapishwa na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) iliyopo katika Wilaya ya Kinondoni, Mtaa wa Kasaba, jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo pia inazalisha Gazeti la MwanaHALISI.

Mhandisi Ngonyani amesema hayo leo jijini Dar es Salaam ambapo amedai kuwa, habari iliyotolewa katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo la tarehe 4 Agosti, 2016 ililenga kumtumia kama daraja la kumchafua Rais John Magufuli.

“Gazeti la Mseto lililotoka Alhamisi iliyopita katika ukurasa wake wa mbele uliweka picha yangu, na jinsi ilivyowekwa watu wengi wamenunua gazeti hilo wakidhani kuwa, habari yake ilikuwa ni kweli,” amesema na kuongeza;

“Habari hiyo si ya kweli ni ya uchafuzi, imeniandika mimi kuwa, nimeandika barua ya kushukuru kupokea fedha katika shughuli za kampeni ya ubunge katika jimbo langu la Namtumbo, na sehemu ya fedha hizo nilizipeleka kwa rais ili kusaidia katika kampeni za uchaguzi.”

Ngonyani amedai kuwa, habari hiyo ni ya kutungwa na kwamba, mwandishi wa habari hiyo alifanya makosa kwa kuandika majina halisi wakati habari ilikuwa ni hadithi ya kutungwa.

“Wamewachafua wawekezaji, mimi nimechafuliwa, na rais pia amechafuliwa, nilikuwa sipo hapa nimerudi nimemaliza kazi yangu nikasoma hilo gazeti, nimeelewa lengo lao ni kutaka kunichafua,” amesema.

Amesema, atawachukulia hatua waliohusika kuandika na kuichapa barua hiyo ili wajue kuwa wanapoandika na kuchapisha habari za kutunga wasitumie majina halisi.

“Itabidi niwachukulie hatua ili na wenyewe wapate stahili yao ya kutumia majina halisi katika hadithi za kutungwa.

“Hayo ni matumizi mabaya ya mtandao na kompyuta tutaendelea kupiga vita, tutawapeleka mahakani mwandishi Josephat Isango, hali halisi publisher na mchapishaji.

Ngonyani amesema, hii itakuwa fundisho kwa waandishi wengine wanapotaka kupata kitu watumie njia sahihi.

“Tumewapa notisi ya siku saba jana mchana, notisi hiyo inasema wakanushe walichoandika na wakiweke front page (ukurasa wa mbele) kama hiyo taarifa ya uzushi walivyoweka, walipe fidia ya shilingi bilioni moja vinginevyo tutalipeleka suala hilo mahakamani.

“Uchafuzi huu umewaathiri wapiga kura wangu, familia yangu, na historia ya rais inapingana na kauli aliyoitoa kwa wafanyabiashara hakuna aliyejitokeza kusema kuwa kuna mtu alimchangia, hii stori inamaanisha kwamba rais aliongea uongo.”

Ngonyani amedai, walioshiriki katika uchaguzi wanajua hawakutumia fedha na kwamba, inakuwaje leo hii waje wasikie kuwa alipata fedha “hawatanielewa na hasa wale waliojitolea kunisaida katika kampeni.

“Fedha hiyo itasaidia kujenga Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo, hiyo bilioni moja itaenda kufanya kazi hiyo,” amesema na kuongeza;

“Ujenzi wa hospitali unahitaji bilioni 10, tuatendelea kuiomba serikali kidogokidogo hadi hiyo fedha itakapokamilisha.”

 

error: Content is protected !!