July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waziri afunga kiwanda na faini Sh. 25 milioni

Spread the love

NAIBU Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, amekifunga na kukipiga faini ya Sh. 25 milioni, kiwanda cha kusindika ngozi mjini Shinyanga cha Xing Xua kutokana na ukiukwaji wa kanuni na sheria za Mazingira ya mwaka 2004. Anaandika Moses Mseti, Shinyanga … (endelea).

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia wa kichina kimefungwa baada ya kubainika kinaendesha shughuli zake huku kikiwa hakijakamilika, pamoja na mazingira yake yakiwa yana hatarisha afya za wafanyakazi pamoja na wananchi wanaokizunguka.

Hata hivyo kiwanda hicho kinachozalisha ng’ombe 2580 na mbuzi na kondoo 1,000 kwa siku kimetelekezwa na wamiliki wa kiwanda hicho kutokana na upatikanaji wa ngozi kuwa mdogo pamoja na kupanda kwa gharama ya ngozi kutoka kwa wachinjaji.

Akizungumza jana mara baada ya kumaliza kufanya ziara ya kukagua kiwanda hicho, Mpina amesema kuwa kiwanda hicho kimekiuka sheria za uendeshaji pamoja na mazingira ya kiwanda hicho kuwa machafu, kitendo ambacho kinahatarisha uhai wa wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho.

Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu, amesema kuwa mara nyingi wawekezaji wamekuwa wakishindwa kufuata taratibu za uendeshaji wa shughuli zao, na wakati serikali ikitaka kuwachukulia hatua hudai kwamba wananyanyaswa bila kutambua kwamba wao ndiyo chanzo cha yote.

“Kwa mamlaka niliyonayo na kwa mjibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004, natamka kwamba kiwanda hiki kuanzia sasa nakifunga kwa muda kutokana na kukiuka Sheria ya Mazingira mpaka pale kitakaporekebisha makosa yaliyopo kwenye kiwanda hiki na wakishindwa kufanya hivyo hatua zitachukuliwa kwa wamiliki wa kiwanda.

“Pia kuna sehemu ya shimo ambalo limerundikwa uchafu uliochanganyikana na vipande vya ngozi, nyama na maji yenye sumu natoa siku saba eneo hilo liwe limefunikwa maana ni hatari kwa afya ya binadamu, na matengeneze maeneo ya kitaalamu ya kuhifadhia taka ngumu na siyo kuzitupa ovyo,” amesema Mpina.

Mratibu wa (NEMC) Kanda ya Ziwa, Anna Masasi, amesema kiwanda hicho kiliomba kibali cha kuchinja mifungo lakini cha kushangaza kinafanya kazi ya kusindika ngozi kinyume na Cheti chao cha uwekezaji hapa nchini, huku akikitaka kibadili cheti hicho kabla ya hatua kuchukuliwa.

Mwenyekiti wa Mtaa Mpera ‘C’ Kata ya Ibadakuli mjini, Charles Sandu, amesema kuwa eneo la kiwanda hicho limekuwa likitoa halufu mbaya na kwamba endapo hatua zisipochukuliwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo wanaweza kuungua ugonjwa mbalimbali huku wakimpongeza naibu huyo kwa hatua ya kukifunga kiwanda hicho.

error: Content is protected !!