May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wazee Chadema wamweka mtegoni Rais Samia

Spread the love

BARAZA la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeishauri  Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ifanye marekebisho ya Katiba ili nchi iwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumapili tarehe 9 Mei 2021, na Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Susan Lyimo, akizungumza na wanahabari mkoani Dar es Salaam, kuhusu hotuba aliyoitoa Rais Samia, katika mkutano wake na wazee wa mkoa huo.

Katika hotuba hiyo aliyoitoa  tarehe 7 Mei 2021, kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Rais Samia alisema Serikali yake hivi karibuni itafanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi, huku akigusia kwamba, atateua watu kutoka vyama vya upinzani, ili kuleta umoja wa kitaifa.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Akizungumzia kauli hiyo,  Lyimo amesema ili azma yake hiyo itimie Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuwe na msingi bora kwa ajili ya kuondoa mgongano wa kimaslahi baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama husika watakapotoka watu wanaoteuliwa.

“Zanzibar kuna kitu kinaitwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ndiyo maana makamu wa rais anatoka upinzani. Wameweka utaratibu kuunda serikali hiyo , lakini bara hatuna utaratibu huo.  Kwa kuwa suala hilo liko kikatiba, kama  ana lengo hilo  tunaomba uwepo wa mabadiliko makubwa ya katiba na sheria,” amesema Lyimo.

Mwanasiasa huyo amesema “ katiba iweke msingi wa kuwa na Umoja wa Kitaifa ili anapoteuliwa asiwe na mgongamo wa kimaslahi, asilazimike kuahama chama.”

Mwanasiasa huyo amesema, kama mabadiliko hayo ya Katiba hayatafanyika, Wazee wa Chadema wanaomba teuzi hizo zisifanyike.

“Zile nafasi anazo ona zina mgongano wa kimaslahi na vyama husika, kwamba mteuliwa itabidi ahame chama, tunaomba teuzi hizo zisifanyike labda kama kutakuwa na marekebisho ya sheria,” amesema Lyimo.

error: Content is protected !!