October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wazee ACT-Wazalendo waomba kuonana na Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

NGOME ya Wazee wa Chama cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania, imeomba kuonana na Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, ili kuzungumza changamoto zinazowakabili. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo tarehe 1 Oktoba 2021 na Mwenyekiti wa Ngome ya ACT-Wazalendo, Yasini Mohammed, kupitia taarifa yake kuhusu maadhimisho ya siku ya wazee duniani, inayoadhimishwa Oktoba Mosi kila mwaka.

Mohammed amemuomba Rais Samia, atenge muda wa kuzungumza na wazee wa vyama vya upinzani, kama alivyokutana na Wazee wa Chama chake Cha Mapinduzi (CCM).

“Aidha, sisi Ngome ya Wazee wa Act Wazalendo, tunasikitishwa kwamba wazee wanaotokana na vyama vya upinzani, hatujawahi kupata nafasi ya kukutana na Mkuu wa nchi. Kwa sababau hiyo, tunashauri Rais atenge muda, awe anakutana na wazee wa vyama vyote kwakuwa ndiyo walezi wa viongozi wote,” amesema Mohammed.

Pia, Mwenyekiti huyo wa Wazee ACT-Wazalendo, ameiomba Serikali ianzishe bima ya afya ya wazee, ili kundi hilo lipate matibabu ya uhakika.

“Tunaona Serikali haijawathamini ipasavyo na kuwapa kipaumbele kinachostahili wazee, licha ya kuwapo wizara mahsusi kwa ajili yao.”

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

“Kwenye eneo hili wazee hawajaandaliwa bima ya afya mahsusi, ambazo zingetoa uhakika wa matibabu yao, kwani bima zilizopo zina gharama kubwa ambazo wazee hawawezi kumudu kuzilipia,” amesema Mohammed.

Wakati huo huo, Mohammed amemuomba Rais Samia awape msamaha wafungwa wazee wanaoendelea kutumikia vifungo katika magereza mbalimbali nchini.

Pia, ameomba Serikali iunde baraza la wazee, litakalowaunganisha wazee wote nchini bila kujali itikadi za kisiasa, kidni na ukabila.

“Mwisho lakini kwa msisitizo mkubwa, Sisi wazee wa Ngome ya ACT Wazalendo, tunatoa wito kwa wazee wote nchini kwenda kupata chanjo ya Uviko -19, kwakuwa wazee tupo kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa maradhi hayo. kuliko kundi lingine lolote,” amesema Mohammed.

error: Content is protected !!