WAZAZI na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chief Kidulile wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi na ukarabati wa madarasa katika shule hiyo ambayo huchukua idadi kubwa ya wanafunzi wilayani Ludewa. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Hayo yameelezwa na baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwandishi wetu kuhusu maboresho ya shule hiyo iliyopo katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Mmoja wa wanafunzi hao, Dorcas Boniphace amesema mazingira ya zamani madarasa waliyokuwa wakiyatumia yalikuwa hayamshawishi mwanafunzi kusoma kwa utulivu.
Amesema muda mwingine wanafunzi walikuwa wanapata shida kupata ufaulu mzuri kwenye masomo kutokana na madarasa yalivyo.
“Milango haikuwepo, ilikuwa unaweza kuingilia mlangoni na kutokea dirishani,” amesema Dorcas na kuungwa mkono na mwanafunzi mwenziye Fadhili Andrew.
Andrew amesema ujio wa madarasa hayo mapya chini ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan yatawasaidia sana kupandisha ufaulu wao.
“Moja ya sababu ambayo huwa inachangia ufaulu wa wanafunzi ni miundombinu ya shule” amesema.
Aidha, mmoja wa wazazi wa wanafunzi katika Shule hiyo ambayo ipo mjini Ludewa, Monica Mchilo amesema awali walikuwa wanachangishana kujenga madarasa kwa nguvu za wananchi.
“Kwa maana ya matofali, mchanga na mawe lakini ni kweli kwamba kwa nguvu za wananchi tusingeweza kufikia kiwango hiki.
“Tunampoingeza na kumshukuru sana Rais Samia kwa sababu ni mama wa pekee kama waswahili wanavyosema ‘hakuna kama mama’,” amesema.
Leave a comment