Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wazanzibari waoneshwa ya 2035
Habari za SiasaTangulizi

Wazanzibari waoneshwa ya 2035

Spread the love

CHAMA cha ACT Wazalendo kimebuni utaratibu mpya wa kujisogeza kwa umma mapema hata kuliko kawaida ya uendeshaji siasa nchini Tanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Huku kikiwa hakijaitupa dhamira yake ya kuipaisha Zanzibar kimaendeleo hadi kufanana na Singapore, nchi ndogo katika Mashariki ya Mbali iliyopiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kipindi kifupi baada ya kupata uongozi mzuri, kinataka kuaminika kwa utendaji maridhawa.

Mbele ya hadhara iliyojumuisha viongozi wa ngazi ya juu hadi matawi, kutoka Unguja, Pemba na Dar es Salaam, kumezinduliwa kile kiitwacho Ahadi yetu kwa Wazanzibari ifikapo mwaka 2035.

Chama hicho kinakisudia kuonesha wananchi na ulimwengu mzima kuwa kinauwezo wa kuijenga Zanzibar yenye uchumi imara, jamii yenye mshikamano na inayijiendesha chini ya Mamlaka yake kamili.

Msemaji mkuu wa mpango huo uliozinduliwa kwenye Hoteli ya Verde, Mtoni mjini Zanzibar, alikuwa Othman Masoud Othman (OMO), Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo.

Akiwa pia ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman alisema chama kimejipanga kuwatumikia Wazanzibari kupata maisha mazuri yaliyo nafuu bali pia kuwa na uhakika wa tiba nzuri, elimu bora kwa watoto wake na maji safi na salama.

“Kupitia mpango wetu, hatusubiri kuja uchaguzi ndipo tuseme hii ilani yetu na tukainadi. Tunayaweka hadharani muyaone yale tunayokusudia kuyatekeleza miaka kumi mpaka ifikapo 2035. Sisi ni chombo makimi cha kisafiria na tutatoa nahodha hodari na muadilifu,” alisema.

“Vuta taswira bila kujali itikadi wala kipato upo chomboni. Jiulize nahodha yukoje, anaendesha vizuri au ni kama injini imetolewa. Sasa safari ya kuifikia Zanzibar yenye maendeleo ina uhakika hapo?”

Alisema, “unajiuliza Nahodha ana dira. Anafahamu twendako. Tunaona safari yenyewe katika chombo abiria wamegawanyika… usalama shida, unafanya biashara mara mlango umefungwa na ZR*, vifaa vimekamatwa na Manispaa. Maji shida, haya ndo maisha kweli?”

“Tunaweka sera bora za kiuchumi zinazoaminika, kutekelezeka na zilizotulia. Uendeshaji nchi kwa Katiba mpya inayojenga misingi ya uwajibikaji dhidi ya ulaji rushwa na uzembe. Unakuwa na viongozi wenye maadili sio mlango wa duka,” alisema.

Alisema kihistoria Zanzibar ni kitovu cha biashara lakini haijafanikiwa kwa kukosekana sera nzuri na uongozi unaojitegemea kimipango na sera na sheria za fedha zilizo bora. “Tutapigania kujitosheleza kwa nishati maana raslimali tunazo, na nishati iliyo rafiki wa mazingira. Kwa jumla Mzanzibari abakie na haiba yake, mwenye afya bora, hifadhi ya jamii na maisha nafuu huku serikali ikisimamia kudhibiti mfumuko wa bei usiathiri maisha yake,” alisema.

Othman alisema chini ya serikali ya ACT, patajengwa mshikamano na maridhiano ya jamii huku masikilizano, mashirikiano na kurudisha desturi ya kusaidiana badala ya hali ya sasa ya maisha ya mwenyenacho na wengi wasionacho.

“Kila mwananchi atatumia uwezo na kipawa chake kuishi na hakutakuwa na kubaguana. Zanzibar ya 2035 haitakuwa ya kubaguliwa. hakuna matabaka kwa kutazama itikadi ya siasa, aila, dini au rangi ya mtu na kule atokako,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama, Juma Duni Haji alisema hayo yanawezekana kwa sababu historia ya vyama vingi nchini inaonesha viongozi wa upinzani Zanzibar wamejitoa na kujitolea mhanga kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi walio wengi.

Duni alisema viongozi wa chama hicho wanaaminika na kwa hivyo wananchi wanayo sababu kuwaamini kwa ajili ya kujihakikishia mustakabali wa maisha yao.

Akihitimisha uzinduzi uliohudhuriwa na baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo CCM, viongozi wa dini na asasi za kiraia, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe alisema chama kimeweka sokoni bidhaa zake; wengine nao waweke zao ili wananchi wachague “bidhaa iliyo bora.”

Katibu Mkuu Ado Shaibu Ado alianzisha uzinduzi kwa kusema chama kimebuni mpango wa kutosha kujenga imani kwa wananchi na wao kuamini kule wanakokusudiwa kuyapeleka matamanio yao.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!