June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wavuvi Muleba wataabika na uhalifu

Wavuvi wakiwa wameegesha mitumbwi yao baada ya kutoka kuvua samani baharini

Spread the love

KWA asilimia kubwa, wakazi wa kanda ya Ziwa hususani mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza, wanategemea mazao yatokanayo na shughuli za uvuvi ili kuendesha maisha yao ya kila siku. Anaandika Ashura Jumapili, Bukoba (endelea).

Shughuli za uvuvi pia ni tegemeo kubwa la ajira katika sekta isiyo rasmi kwa makundi mbalimbali ambayo pia yanachangia ukuaji wa uchumi wa taifa na hali hiyo inajidhihirisha katika visiwa tofauti kwenye Ziwa Victoria.

Pamoja na umuhimu wa sekta ya uvuvi, changamoto nyingi zinazoibuka kila mara bila kutafutiwa ufumbuzi ni kielelezo cha eneo hilo kutopewa kipaumbele sana na Serikali kama zilizvyo sekta nyingine hapa nchini.

Licha  ya  kutopewa kipaumbele,bado sekta ya uvuvi ni tegemeo kubwa kwa baadhi ya halmashauri ambazo hutegemea shughuli zitaokanazo na uvuvi kama vyanzo vikuu vya mapato kama inavyojidhihilisha katika Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kuwa jumla ya wavuvi 22,930 ambapo tangu mwaka 2008 hadi 2012, Sh. 3.8 bilioni zilikusanywa kama maduhuli kupitia tozo mbalimbali za biashara halali ya uvuvi.

Pia, mipango ya maendeleo katika halamshauri zinazotegemea uvuvi kama sehemu ya vyanzo vya ndani vya mapato inaonekana kutozingatia umuhimu wa kuboresha vyanzo hivyo, ikiwa ni pamoja na kuwezesha mikakati ya kuwepo uhakika wa ulinzi na usalama kwa wavuvi.

Matukio ya mara kwa mara ya utekaji wa boti na uporaji wa mali za abiria wanaosafiri katika visiwa mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria ni uthibitisho wa kulegalega kwa suala la usalama na hivyo kudhoofisha shughuli za uchumi zinazotegemea uvuvi.

Ukubwa wa tatizo

Baadhi ya wavuvi kutoka visiwa tofauti kwenye Ziwa Victoria, wanaelezea vitendo vya ujambazi kama uhalifu unaokwamisha shughuli zao za kujikwamua huku kwa upande wa pili, shughuli wanazofanya zikitegemewa kuchangia uchumi wa taifa.

Miongoni mwa waathirika wa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha ni Misana Ramadhani, mkazi wa mwalo wa Kimoyomoyo katika kijiji cha Mazinga; anasema anashangaa ukimya wa serikali pamoja na kukithiri kwa matukio hayo.

Anaelekeza lawama zake kwa Jeshi la Polisi kuwa pamoja na kufahamu kuwepo kwa matukio hayo hakuna jitihada za wazi zinazochukuliwa, mazingira yanayowafanya waporaji waendelee kutamba ziwani.

“Majambazi wamekuwa wakifanya uporaji kila wanapojisikia kwa kuwa wanajua jeshi la polisi wilayani hapa haliwezi kufanya chochote pamoja na kujua kuwa matatizo hayo kwa wavuvi yapo na yanatokea kila mara’’anasema

Ramadhani.

Anaongeza kuwa, katika tukio la hivi karibuni, wavuvi watano walijeruhiwa kwa kukatwakatwa kwa mapanga na kuporwa zana zao za uvuvi zenye thamani zaidi ya Sh. 60 milioni.

Anawakumbuka waliojeruhiwa kuwa ni Nicholaus Cleophas ( 33 ), Amidu Hussein ( 32 ), Mussa Antony (28 ), Medson Muhanika ( 30 ) na Juma Said (40) ambao wote ni wakazi wa Mulumo katika kisiwa cha Mazinga.

“Mimi nimeibiwa zaidi ya mara tatu ikiwemo mitumbwi na injini, sasa sisi ni kundi lililosahaulika na na tunaonekana kutokuwa na uhuhimu wowote pamoja na kuwa tunategemewa kuchangia shughuli za kiuchumi,’’anabainisha.

Hali ya kutokuwepo kwa usalama wa uhakika pia ilisababisha hivi karibuni baadhi ya wavuvi katika kisiwa cha Mazinga, kuandamana hadi kwenye kituo cha polisi wakihoji kufumbiwa macho kwa uhalifu unaoendea bila kupatiwa ufumbuzi.

Wavuvi hao walikosoa utaratibu wa doria wakisema unaambatana na unyanyasaji dhidi ya wavuvi vikiwemo vitendo vya vitisho vinavyozidisha hofu na kuleta wasi wasi juu ya dhamira ya dhati ya kudhibiti uhalifu ziwani.

Miongoni mwa wavuvi waliowahi kuvamiwa na kuporwa mali ni Majura Khamis, mkazi wa kisiwa hicho, ambaye anasema akiwa na wenzake walivamiwa na kundi la watu wenye silaha na kuporwa zana zao za uvuvi.

 

“Baada ya kututishia kwa silaha, tuliporwa injini za mitumbwi sita zenye thamani ya zaidi ya Sh.18 milioni, ambapo wenzetu sita walijeruhiwa vibaya kwa mapanga bila kupata msaada wowote,’’ anasema Khamis.

Khamis analalamika kuwa, vitendo hivyo vya uhalifu ziwani vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya wavuvi na kuwafanya kuendelea kuwa masikini badala ya kupiga hatua zaidi ya maendeleo.

Naye Thomas Josia, ambaye ni mmiiki wa mitumbwi, anasema wakati wa kutoza kodi, serikali inakuwa makini kuwafuatilia ingawa uharaka huo hauonekani wanapohitaji msaada wa kuokoa mali zao zinazoporwa ziwani.

Anasema ni vyema serikali isaidie kuwakomboa kwa kuwapatia huduma muhimu hasa watu wanaofanya sekta binafsi za uvuvi ambao ndio kimbilio la kukusanyiwa ushuru na tegemeo kubwa la ajira kwa makundi mbalimbali kwenye jamii.

Bushir Hussein ni mfugaji maarufu wa samaki mkoani Kagera, ambaye anakumbuka changamoto za hali mbaya ya usalama kwenye ziwa Victoria kabla ya kuanza kujishugulisha na kazi hiyo alipoona samaki wanazidi kupungua katika ziwa hilo.

Anasema pamoja na kuwa ameamua kujihusisha na ufugaji wa samaki badala ya kuhangaika kuwatafuta kwenye ziwa lenye changamoto kubwa za kiusalama, bado anaiomba serikali kuangalia upya mfumo wa kulinda maisha ya wavuvi na mali zao.

Kisiwa cha Goziba nacho kina kumbukumbu nyingi za matukio ya uhalifu kama ilivyo katika visiwa vingine wialayani Muleba. Bado tukio la uhalifu mkubwa la Julai 2012, halijafutika vichwani mwa wavuvi. 

Milton Kibiki, aliwashuhudia watekaji wenye silaha waliofika wakiwa na boti yenye mwendo wa kasi muda wa mchana na kuwaweka wakazi wa kisiwa hicho chini ya ulinzi. 

Anasema baada ya kuwekwa chini ya ulinzi kwa saa kadhaa, majambazi hayo yalichukua kila yalichokihitaji.

Sasa matukio hayo ya uhalifu yamewafanya wavuvi kuamua kutafuta ulinzi wao binafsi ambao wanawakodi kutoka jijini Mwanza katika makampuni mbalimbali.

Kwa mujibu wa Milton Kibiki, ambaye pia ni kiongozi wa kusimamia mazingira ya mwalo (BMU) katika kisiwa hicho, kila mwezi wakazi wa Goziba hulipa Sh. 6 milioni kwa ajili ya kugharamia ulinzi. 

Mkuu  wa Polisi wa majini Mkoa wa Kagera ( OC  MARINE), Alex Mkonda, amesema matukio hayo yalikuwa yakitokea miezi michache iliyopita na hivi sasa yameshadhibitiwa.

Anaongeza kuwa baada ya matukio hayo, jeshi  la   polisi   mkoani  humo lilianda mkakati wa kumaliza tatizo la  utekaji  majini na  uporaji wa mali za abiria na wavuvi.

error: Content is protected !!