August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wauza nywele zao kukabiliana na umasikini

Spread the love

HALI ni tete kwa wananchi wa Venezuela kufuatia ugumu wa maisha unaochochewa na mfumuko wa bei unaolikumba taifa hilo kwa sasa, anaandika Wolfram Mwalongo.

Katika kukabiliana na ugumu wa maisha, wananchi hao sasa wamelazimika kuanza kuuza nywele zao ili kujipatia fedha za kujikimu kwa mahitaji ya kila siku ikiwemo chakula na matibabu.

Wananchi wa Venezuela waishio mpakani na nchi ya Colombia ndiyo wanaoongoza kwa kuuza nywele zao katika nchi hiyo jirani.

Huduma muhimu za kibinadamu zinazidi kuwa adimu huku kukosekana kwa madawa na chakula ikiwa ni mojawapo ya mambo yanayotajwa kuchochea hisia za wananchi kumtaka Rais Nicolas Maduro wa taifa hilo kuachia ngazi.

Celina Gonzales mwenye miaka 45 akifanya mahojiano na Shirika la Habari la Reuters, amesema alifanya uamuzi wa kuuza nywele ili kununua dawa ya kutibu ugonjwa unaosababishia maumivu kwenye maungio ya mifupa (Arthritis).

“Nimekuwa nikisumbuliwa na ugonjwa unaonisababishia maumivu makali kwenye maungio ya mifupa kwa muda mrefu sasa, kutokana na kukosekana kwa fedha za matibabu nililazimika kuvuka mpaka kwenda kuuza nywele ili niweze kupata dawa za kutuliza maumivu,” amesema.

Mwanamke huyo aliuza mafungu ya nywele zenye thamani ya Dola 20 za Marekani sawa na Sh. 43,670/= za Tanzania.

Wakati hali ikizidi kuwa ngumu katika taifa hilo Rais Maduro anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wananchi wake ambao wanamtaka kung’oka Ikulu kutokana na kuzidi kuangusha uchuni wa nchi hiyo.

Wapinzani wake wa kisiasa wameendelea kuchochea maandamano nchini humo ambapo maelfu ya raia wa Venezuela waliandamana katika maeneo mbalimbali tarehe 26 Oktoba mwaka huu  wakiitikia wito wa upinzani.

Muungano wa upinzani (MUD) umeendelea kumshinikiza kiongozi huyo kundoka Ikulu kwa kushindwa kusimamia uchumi hali inayosababisha taifa hilo kuendelea kuelea katika lindi la umaskini.

Wakati hali ikizidi kuwa tete madereva wa mabasi katika mji wa Caracas wiki iliyopita waliitisha mgomo, wakipinga ongezeko la nauli na gharama za vifaa  vya magari kitendo hicho kilisababisha adha kubwa ya usafiri katika mji huo mkuu wa Venezuela.

Hugo Ocando, msemaji wa madereva hao amesema takribani madereva 25,000 wanaunga mkono mgomo huo.

error: Content is protected !!