August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waumini wamgomea Askofu wao  

Spread the love

HALI si shwali katika Kanisa la AICT Mkolani lililopo katika Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza baada ya baadhi ya waumini kugomea hatua ya John Bunango, Askofu wa kanisa hilo Jimbo la Mwanza kumuhamisha Mchungaji Marko Moshi, anaandika Moses Mseti.

Mchangaji huyo anayetaka kuhamishwa na Askofu Bunango kwa sasa ni mgonjwa na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), Mwanza kuokana na maradhi ambayo hayajatajwa.

James Ngoi ambaye ni miongoni mwa viongozi wa kanisa hilo akizungunmza kwa niaba ya waumini wenzake amesema, waumini wamemgomea askofu wao kumhamisha Mchungaji Moshi na kupelekwa Mallya wilayani Kwimba kwa madai ya kuwa na matatizo ya kiafya yanayomkabili.

Amesema, wanashangazwa na kitendo cha askofu huyo kutana kumhamisha Mchungaji Moshi kwenda Mallya wilayani Kwimba huku hali yake ya kiafya ikiwa tete.

“Mchungaji Moshi hivi sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) akisumbuliwa na maradhi ya upungufu wa damu mara kwa mara.

“Sisi waumini tunapata hofu kwa sababu anaweza kupoteza maisha endapo atapelekwa huko kijijini ambako hakuna huduma nzuri ya hospitali,” amesema Ngoi.

Ngoi hata hivyo amesema, kwa niaba ya waumini hao Mchungaji Moshi amekaa katika kanisa hilo kwa muda wa miaka sita sasa, huku akifanikisha kulilea kiroho kanisa hilo.

Amesema, wananchi hawapendi kuona mchungaji huyo anahamishwa na kupelekwa huko kutokana na hali yake kiafya kutokuwa nzuri, hivyo kupelekwa kijijini ni kuhatarisha usalama wa afya yake.

“Tunamuomba Askofu Bunango amuache mchungaji wetu aendelee kuliongoza kanisa letu, ingawa ni haki kuhamishwa lakini uamuzi unaochukuliwa wa kumuondoa unaonekana ni kumkomoa licha ya afya yake kuwa si nzuri,” amesema.

Zawadi Masanja, ambaye ni muumini wa kanisa hilo amesema, kwa sasa hawana mpango kuona mchungaji wao anahamishwa ama kumpokea mchungaji mwingine.

“Hali hii itasababisha kuwapo na mafungu mafungu kanisani, hivyo ili hali iwe vizuri inatakiwa Askofu Bunango amuache mchungaji wetu kutokana na afya yake kutokuwa njema,” amesema Masanja.

Joel Ng’weng’weta, Katibu wa Dayosisi hiyo alipotafutwa na mtandao huu kuzungumzia suala hilo, alidai hana la kuzungumza na kwamba, yeye hawajibiki kwenye vyombo vya habari.

error: Content is protected !!