Wednesday , 29 March 2023
Home Gazeti Habari Watumishi wavunja agizo la Magufuli, wasakwa
Habari

Watumishi wavunja agizo la Magufuli, wasakwa

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania
Spread the love

 

WATUMISHI waliogoma kuhamia kwenye maeneo ya halmashauri zao, wamevunja agizo la Rais John Magufuli hivyo, wasakwe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Waziri Majaliwa ametoa agizo hilo leo Alhamisi tarehe 4 Februari 2021, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, bungeni jijini Dodoma.

Amesema, wapo watumishi ambao hadi sasa hawajahamia katika maeneo yao mapya ya kazi, na kwamba wanavunja Sheria ya Utumishi wa Umma kwa kukaidi agizo la Rais John Magufuli, liliowataka kuhamia kwenye maeneo hayo mara moja.

“Na hii ilikuwa ni agizo la mheshimiwa rais na agizo la rais ni agizo ambalo inatakiwa litekelezwe mara moja, kutokwenda ni kuvunja amri, kukataa amri ya rais ni kosa kubwa sana kwenye utumishi wa umma,” amesema Waziri Majaliwa.

Hivyo, Waziri Majaliwa ametoa siku mbili kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kumpa orodha ya Halmshauri za Wilaya ambazo watumishi wake wamegoma kuhamia katika vituo vyao vipya vya kazi, ili awachukulie hatua.

Ameagiza TAMISEMI kufuatilia halmashauri zilizotakiwa kuhama kwenye maeneo yao ya zamani na kwenda katika maeneo mapya, kisha ifikishe taarifa hizo ofisini kwake Jumamosi ya tarehe 6 Februari 2021.

Joseph Msukuma, Mbunge wa Geita Vijijini

“Nitahitaji taarifa hizo keshokutwa Jumamosi ofisi kwangu saa nne, ili nijue halmashauri gani ambazo watumishi hawajahama ili nichukue hatua za kinidhamu kwa watumishi hao,” ameagiza Waziri Majaliwa.

Watumishi hao wanaodaiwa kugoma kwenda katika maeneo yao mapya ya kazi, wengi wao ni wale wa halmashauri za wilaya ambazo ofisi zake zimehamishwa kutoka mjini kwenda vijijini.

Waziri Majaliwa amesema, Rais Magufuli alitoa agizo hilo ili kuhakikisha huduma zinasogezwa karibu kwa wananchi.

“Ni kweli rais alitoa maagizo kwa halmashauri za wilaya zote ambao zilikuwa na makao makuu yake kwenye makao makuu ya halmashauri za miji, kuhama mara moja na kwenda kwenye makao makuu huko ambako wananchi walipo ili waweze kuwahudumia kwa ukaribu,” amesema Waziri Majaliwa.

Sambamba na hilo, Waziri Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa ambao halmashauri zimehamishwa, kuhakikisha watumishi wa halmashauri hizo wanakwenda katika maeneo yao mapya mara moja.

“Nataka niwaagize wakuu wa mikoa akiwemo na mkuu wa mkoa, katibu tawala wa mkoa ambaye ni mtendaji mkuu kwenye mkoa huo, ambao kwenye halmashauri zenye mazingira hayo ambayo watumishi wanatakiwa kwenda kwenye makao mapya hawajaenda, waondoke mara moja.

“…na endapo hawatafanya hivyo, mkuu wa mkoa husika achukue hatua mara moja dhidi ya watumishi hao na hasa wale wote ambao hawataki kwenda kwenye maeneo mapya.”

Amesema, watumishi hao hawataongewea muda wa kuhamia katika maeneo yao mapya ya kazi, kwa kuwa kipindi kilichotolewa kimeshaisha.

“Kwa sababu kipindi cha kuondoka kilishatamkwa na mheshimiwa rais, hawa hatuna sababu ya kuwapa muda tena.  Ni kuondoka mara moja baada ya tamko hili,” amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kusheku ‘Msukuma’, aliyehoji kauli ya serikali kuhusu changamoto za baadhi ya halmashauri za wilaya kuingia gharama kuwalipia watumishi wao fedha za usafiri.

Msukumu amesema, halmashauri hizo zinaingia gharama hizo kwa kuwatoa watumishi wake katika maeneo yao zamani (mjini) hadi katika vituo vyao vipya vya kazi (vijijini).

“Kuhama inapelekea halamshauri kuwa na mzigo wa kugharamia mafuta kila siku kurudisha watumishi kulala mjini, ni nini kauli ya Serikali kwenye halmashauri hizo ambao zinarudi vijijini na watumishi wanarusidhwa kulala mjini?” amehoji Msukuma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

ElimuHabari

Serikali yataka vijana  wajiunge na program atamizi ya biashara CBE

Spread the love  SERIKALI imewahamasisha vijana kujiunga na program atamizi inayotolewa na...

AfyaHabari

Ugonjwa wa ajabu ulioua watano Bukoka ni Marburg

Spread the loveWAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa ajabu uliosababisha...

AfyaHabariHabari

Ugonjwa wa ajabu wadaiwa kuua watano Kagera, Serikali yatoa tahadhari

Spread the loveJUMLA ya watu watano wanaidaiwa kufariki dunia  katika vijiji vya...

ElimuHabari

CBE yaanzisha Shahada 10 za Uzamili, CBE yajivunia wahitimu wanaoajirika

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka wenye  kampuni na...

error: Content is protected !!