January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watumishi watakiwa kuwa wabunifu

Afisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) akitoa maelekezo kwenye maonesho ya Wiki ya Watumishi wa Umma

Spread the love

WATUMISHI wa Umma, wametakiwa kuonesha ubunifu na weledi katika kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Rai hiyo imetolewa leo na Hab Mkwizu, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, wakati akifungua ‘Wiki ya Utumishi wa Umma’ jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Celina Kombani, Waziri wa Nchi, Ofsi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “Utumishi wa Umma Katika Bara la Afrika ni Chachu ya Kuwawezesha Wanawake Kuongeza Ubunifu na Kuboresha Utoaji wa Huduma kwa Umma.”

“Kaulimbiu hii ni muhimu kwa nchi yetu kutokana na mchango unaotolewa na wanawake katika Utumishi wa Umma na maendeleo ya nchi yetu na Bara la Afrika,” amesema Mkwizu.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa serikali kuendelea kutekeleza sera na mikakati inayotoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume, ikiwemo kuwajengea uwezo ili wafanye kazi kwa weledi, ushindani na tija.

Aidha, amesema utekelezaji wa miongozo ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Jamii ya Mwaka 1996, Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 na Mwongozo wa Anuai za Jamii wa mwaka 2010, imechangia kuongeza idadi ya wanawake katika maamuzi serikalini kutoka asilimia 26 mwaka 2005 hadi asilimia 34 Mwaka 2014.

“Katika kipindi cha miaka 10, jumla ya watumishi wanawake 251 walipatiwa ufadhili na kuhitimu masomo yao katika shahada za uzamili hii ikiwa ni sifa muhimu kwao kustahili nafasi za uongozi katika Utumishi wa Umma na nje ya Utumishi wa Umma,”amefafanua Mkwizu.

Kuhusu wajibu wa serikali katika kuhudumia wananchi, amesema “mafanikio yanategemea jinsi serikali inavyothamini mchango wa wadau kwa upande mmoja na wananchi kwa upande mwingine.”

Hivyo, amezitaka sekta binafsi na vyombo vya habari kuendelea kutoa mchango katika kuimarisha Utumishi wa Umma katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

error: Content is protected !!