May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watumishi walioondolewa kazini kimamkosa walipwa Sh. bilioni 2.6

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, utumishi na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imelipa madai ya mishahara kiasi cha Sh. 2.6 bilioni, kwa watumishi 1,643, walioondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara kimakosa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 31 Agosti 2021 na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, utumishi na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, bungeni jijini Dodoma.

Akimjibu Mbunge wa Mikumi (CCM), Dennis Londo, aliyehoji idadi ya watumishi waliorudishwa kazini na kulipwa stahiki zao, baada ya kuondolewa kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti feki na wafanyakazi hewa, lililofanyika 2017.

“Serikali imelipa madai ya mishahara ya jumla ya Sh. 2,613,978,035.54 (Sh. 2.6 bilioni), kwa watumishi 1,643 waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa,” amesema Ndejembi.

Aidha, Ndejembi amesema  uhakiki wa madai yaliyobaki unaendelea na kwamba wataendelea  kulipwa kwa kadri yanavyohakikiwa.

Akitaja idadi ya watumishi waliorudishwa kazini, Ndejembi amesema Serikali imewarudisha kazini watumishi 4,380, wakiwemo watendaji wa vijiji na mitaa 3,114.

Wakati huo huo, Ndejembi amesema Serikali imetoa msamaha wa kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kwa kukosa sifa ya elimu ya kidato cha nne na baadae wakajiendeleza na kupata sifa tajwa hadi kufikia Disemba 2020.

“Waliopata msamaha 2020, ni wale  ambao hawakudanganya katika taarifa zao kuwa wana elimu ya kidato cha nne au kubainika kughushi vyeti,” amesema Ndejembi.

Ndejembi amesema, Serikali imewaagiza waajiri kushughulikia hatima za ajira za watumishi, walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya kidato cha nne , ikiwemo malipo ya stahili zao.

error: Content is protected !!