January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watumishi wa umma chanzo cha migogoro ardhi

Spread the love

ANGELINA Mabula, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi inachangiwa kwa kiasi kikubwa na watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu kwenye nafasi zao, anaandika Moses Mseti, Mwanza.

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati mkutano wa hadhara uliowahusisha wananchi wa Kijiji cha Nyamule wilayani Misungwi mkoani hapa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi kwa mikoa ya kanda ya ziwa.

Mabula amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikisababishwa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu ambao wanaendekeza vitendo vya rushwa vinavyosababisha migogoro ya mara kwa mara nchini.

Waziri huyo amesema migogoro ya ardhi ambayo inaendelea kufukuta nchini, ikiwamo ya kijiji cha Nyamule wilayani Misungwi, imesababishwa na baadhi ya watumishi wanaoendekeza vitendo vya rushwa.

Kijiji cha Nyamule kimeingia katika mgogoro wa kugombea mpaka na Taasisi ya Utafiti wa Mimea ya Ukiriguru, baada ya kitengo cha ardhi kushindwa kuainisha mpaka wa kijiji na taasisi hiyo.

Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani hapa, amesema katika uchunguzi aliofanya, amebaini kwamba kuna mchezo `mchafu` unaofanywa na watumishi wa Misungwi kwa lengo la kujiingizia kipato kwa njia za panya.

Hata hivyo amesema kuwa kukosekana kwa mpaka wa kijiji na taasisi hiyo imesababisha wananchi wanaozunguka eneo la taasisi hiyo kushindwa kufahamu eneo lao ambalo lingewasaidia katika shughuli zao.

Amesema kuwa kukosekana kwa mipaka hiyo imesababisha wafungaji kuingiza mifugo yao katika eneo la taasisi hiyo kwa ajili ya malisho na kusababisha mgogoro baada ya wamiliki wake kuanza kutoza fedha pindi wanapokamata mifugo yao.

“Uchunguzi tulioufanya na wananchi wenyewe wamethibitisha suala hilo ni pale ambapo tulipokuta kuna risiti feki ambazo zimetengenezwa na baadhi ya watumishi wa wilaya hiyo kwa lengo kuwatapeli wananchi wanapokamata mifugo yao,” amesema Mabula.

Kufuatia hatua hiyo, waziri huyo ameiagiza wilaya ya Misungwi kufuatilia maeneo yote ambayo hayajapimwa na kuwekewa mipaka kufanyiwa kazi mara moja ikiwamo kijiji hicho cha Nyamule.

error: Content is protected !!