July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watumishi shule za Bakwata Dom, wamlilia Mufti

Spread the love

WATUMISHI na walimu wa shule ya sekondari ya Hijra pamoja na sekondari ya Jamhuri  ambazo zinamilikiwa na Baraza Kuu la Waislam (Bakwata) wamemuomba Mufti wa Tanzania, Shekhe Abuobakari Zuberi kumsimamisha kazi Meneja wa shule hizo, Mashaka Kitundu na ikishindikana  wametishia kugoma kwa muda usiojulikana. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Watumishi hao wamefikia hatua hiyo kwa madai kwamba hawana imani na mkuu wa shule ya sekondari ya Hijra na meneja wa shule ya Hijra na Jamhuri ambaye pia ni Kaimu katibu wa Bakwata mkoa, Mashaka Kitundu, kutokana na manyanyaso wanayoyapata ikiwa ni pamoja na kutolipwa mishahara yao na stahiki nyingine.

Watumishi hao wameiambia MwanaHALISI Online kwa masharti ya kutotaka kutajwa majina walisema, Kitundu amegeuka kuwa mungu mtu kwa kutowasikiliza watumishi shida zao.

Wakizungumzia adha yanayopata watumishi hao walisema ni kutolipwa mishahara yao huku Meneja huyo akiendelea kujineemesha kwa kutumia rasilimali za shule hizo.

Watumishi hao pamoja na walimu walisema kwamba kwa sasa wana hali mbaya kwani hawajalipwa mishahara yao na pale wanapodai wanapigwa kalenda.

“Tangu mwezi Julai hadi mwezi huu, hatujalipwa mishahara, mara tunalipwa Sh. 10,000 na wengine wanapewa Sh. 50,000 na hatujui ni za nini.

“Mbaya zaidi Meneja Kitundu ametugawa watumishi kuwa wale ambao amewafanya watu wake wa karibu huku wengine akiwa hataki hata kuwasikiliza,” amesema mmoja wa watumishi.

Mbali na hilo watumishi hao pamoja na walimu walisema kumekuwepo kwa matumizi ya fedha za shule hizo kwa kile ambacho walisema ni ukiukwaji wa manunuzi.

“Unaweza kuona tangu aje hapa Meneja Kitundu hali ya watumishi imekuwa mbaya lakini jambo la ajabu ni matumizi kuwa makubwa tofauti na kipindi cha nyuma.

“Hivi karibuni alitumia kiasi cha Sh. 800,000 kwa wiki kulisha wanafunzi wa Bweni ambao ni kati ya 150 ambapo kawaida wanafunzi hao wa bweni hutumia 450,000 kwa wiki,” walieleza.

Kutokana na hali hiyo watumishi walimuomba Mufti wa Taifa, Abuobakari Zuberi kumwondoa au kumsimamisha kazi ili uchunguzi ufanyike kubaini ubadhilifu alioufanya kwa muda mfupi tangu afike shuleni hapo.

Katika hatua nyingine watumishi hao walisema, Kitundu amekuwa akiwabeza watumishi kwa maelezo kuwa hakuna mtu wa kumfanya lolote kwani yeye anamahusiano makubwa na Katibu mkuu wa Bakwata Taifa, Seleman Lolila.

Mashaka Kitundu alipoulizwa juu ya tuhuma hizo, alikataa kusema jambo lolote na badala yake alitoa maelekezo ni wapi pa kukutana lakini hakutokea.

Kitundu akutaka kuzungumza jambo lolote juu ya malalamiko hayo na badala yake alitaka kukutana na mwandishi wa habari ili azungumze naye jambo hata hivyo hakulifanya hadi gazeti linapelekwa mitamboni.

Naye Katibu Mkuu wa Bakwata Taifa alipoulizwa kama kweli anamkingia kifua Meneja alisema hahusiki kwa jambo lolote.

“Hivi kweli hayo maneno wewe unayaamini yeye Meneja ndiye anayelipa mishahara na ndiye anayeishi huko Dodoma sasa iweje mimi ebu jaribu kumuuliza vizuri huyo muhusika ila mimi sihusiki,” amesema Lolila.

Alipotafutwa Meneja wa shule hizo, Mashaka Kitundu alipoulizwa juu ya tuhuma hizo watumishi kukosa mishahara alisema tatizo la mishahara katika shule ya sekondari ya Hijra lipo na ni kutokana na kuwepo kwa madeni ya ada kwa wanafunzi.

Hata hivyo amesema kutokana na kutokuwepo kwa fedha amelazimika kuchukua mkopo Benki kwa ajili ya kulipa mishahara ya walimu na watumishi.

“Ni kweli kuna matatizo makubwa katika shule ya Hijra na hali hiyo inatokana na kuwepo kwa walimu ambao hawana viwango ambao ndiyo chanzo kikubwa cha kupiga kelele.

“Kuhusu kwamba mimi natumia jina la katibu mkuu wa Bakwata Taifa ni uzushi na ni fitina”alisema Kitundu.

“Hata hivyo naomba ndugu yangu mwandishi achana na hiyo habari na tukutane ofisini ili tuweze kuweka mambo sawa, wapo baadhi ya waandishi wenzako inapotokea tatizo kama ili tunamaliza mchezo hivyo naona na wewe achana na hilo jambo,” alisisitiza Kitundu.

error: Content is protected !!