August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watumishi hewa wafilisi serikali

Spread the love

 

WATUMISHI hewa 367 kati ya 1057 katika Mkoa wa Mwanza, wamebainika kutafuna zaidi ya Sh. 2 bilioni 2, anaandika Moses Mseti.

Ni wale ambao majina yao yapo katika ofisi lakini wao hawapo katika vituo vyao vya kazi, wengine wakiwa hawatambuliki katika Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri.

Ulipaji wa mishahara watumishi hewa unadaiwa kufanywa na baadhi ya wakuu wa idara na wakuu wa vitengo wasiokuwa waaminifu huku wengine wakituhumiwa kupokea fedha zilizokuwa zikitolewa.

Hayo yamebainishwa na John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mbele ya Susan Mlawi, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma wakati wa maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.

Mongella amesema, kumekuwepo na baadhi ya wakuu wa idara na wakuu wa vitengo mkoani humo wasiokuwa waaminifu ambao wamesababisha kuendelea kuwepo kwa watumishi hewa, kitendo ambacho alidai hakitafumbiwa macho.

Amesema kuwa, katika uhakiki wa watumishi hewa katika mkoa huo, ulioanza Aprili 18 na kumalizika Juni 3 mwaka huu, umefanikiwa kuwapata watumishi hao hewa huku wengine wakiendelea kulipwa mishahara.

“Kuna watumishi wa 13 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Kwimba ambao wamekopa mikopo benki na wakati hawapo katika utumishi wa umma na wanaofanya hayo ni wakuu wa idara.

“Pia kuna watumishi 72 ambao wamelipwa mapunjo ya mishahara katika halmashari ya Wilaya ya Magu kupitia akaunti zao za benki na vilevile wakalipwa tena kupitia dirishani (Double payment) na kila mmoja alikuwa analipwa zaidi ya milioni tatu,” amesema Mongela.

Mongela amesema, kutona na kuwepo kwa watumishi hao, ofisi yake inakusudia kuwafuta watumishi wote wasiojulikana kwa waajiri, kuwafuta kwenye malipo watumishi waliofariki, walioacha kazi waliofukuzwa kazi na waliostaafu.

Wengine watakaofutwa ni waliogombea nafasi tofauti ikiwemo ubunge, kuwachukulia hatua maofisa wa halmashauri waliohusika kuanzisha na kuidhinisha mikopo kwa watumishi waliotoka katika utumishi wa umma.

Hatua nyingine zitakazochukuliwa ni kuhakikisha watumishi waliolipwa mapunjo ya fedha za mishahara zaidi ya stahili zao zinarejeshwa, kuwachunguza na kubaini maafisa na wasimamizi wa watumishi waliosababisha upotevu wa fedha kupitia malipo ya mshahara wa watumishi hewa.

Hata hivyo Mongella amesema, Februari mwaka huu watumishi hewa waliolipwa mshahara katika sekretarieti ya mkoa na halmashauri walikuwa 28,068, halmashauri 27, 416 na katika sekretarieti ya mkoa walikuwa 652 huku watumishi wa halmashauri waliohakikiwa ni 26, 359 ambao hawakufika kuhakikiwa ni 1,057.

Na kwamba licha ya kutolewa kwa tangazo la kuwaita watumishi wote, waliopo masomoni, likizo na waliohama vituo vyao vya kazi lakini wengine hawakuweza kutekeleza agizo hilo jambo ambalo linaonesha wazi ni watumishi hewa.

 

error: Content is protected !!