Spread the love

 

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto na Walemavu, Dk. Dorothy Gwajima ameanzisha utaratibu wa watumishi wa wizara hiyo kujipima wenyewe kupitia mfumo wa kadi ya alama (score cards) katika utendaji wa kazi ili kujenga taasisi itakayokuwa ya mfano. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Dk. Gwajima ameanzisha utaratibu huo ikiwa ni katika kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi na viongozi utakaosaidia kupunguza changamoto mbalimbali zitokanazo na utendaji.

Akizungumza na watumishi wa wizara hiyo leo tarehe 14 Disemba, 2021 jijini Dodoma amewahimiza kujenga tabia ya kufanya kazi kwa ushirikiano na umakini.

Amesema, katika utaratibu huo kutakuwa na mwongozo ambao utatumika kumpima kila mtumishi kutokana na majukumu yake kupitia kadi ya alama jambo litakalosaidia kuongeza kasi ya utendaji katika kuwahudumia wananchi.

“Kila mmoja ajue anafanya nini katika eneo lake kwani hatua ya kwenda kupimana inaanza ili kuchochea tija na kasi katika kutimiza wajibu wetu, tusisubiri wateja tu ndiyo watufanyie tathmini bali tuanze wenyewe, taasisi imara hujengwa kwa maoni imara na ushirikishi na mawazo ya pamoja” ameongeza Dk. Gwajima.

Aidha, Dk. Gwajima ametumia fursa hiyo kuchukua maoni ya watumishi wote kupitia zoezi la ujazaji wa karatasi isiyotaja taarifa yoyote ya mjazaji lengo ni kujua mawazo ya watumishi katika kujenga taasisi ili ilete tija katika utoaji huduma kwa wananchi na kuwa taasisi ya mfano wa kuigwa.

Hata hivyo, Dk. Gwajima amesisitiza kuwa mfumo wa kutumia maoni ya watumishi katika uendeshaji wa taasisi hiyo utakuwa endelevu, kwani hutoa fursa ya kupata mawazo tofauti katika kuboresha utoaji huduma.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dk. John Jingu amemshukuru waziri huyo kwa utaratibu huo ambao amesema ni nadra katika taasisi kwa viongozi kupimana.

“Ni jambo la kihistoria kuwa na utaratibu huu kwani utasaidia kuwajenga watumishi wote kuwa na mtazamo mmoja kuanzia ngazi ya uongozi, mara nyingi viongozi huwa hawafahamu hali halisi ya changamoto za watumishi wa chini yao” amesema Dk. Jingu.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Sichalwe amemshukuru Dk. Gwajima kwa ubunifu aliouanzisha, huku akiwataka watumishi waliojitokeza kuitumia fursa hiyo kama sehemu ya maboresho ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *