SERIKALI ya Tanzania imesema, watumishi 1,496 wanakaimu nafasi za uongozi katika taasisi mbalimbali zikiwemo halmashauri za wilaya na sekretarieti za mikoa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kati ya watuhumishi hao, 332 wanakaimu nafasi zao wakiwa na vibali halali kutoka kwa katibu mkuu utumishi na watumishi 1,164 wanakaimu nafasi zao bila kuwa na vibali.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, tarehe 18 Juni 2021 na Naibu Waziri-Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi wakati akijibu swali la Mbunge Kibamba (CCM), Issa Mtemvu (CCM), bungeni jijini Dodoma.
Mtemvu aliulizwa “ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukaimu muda mrefu kwa watumishi kwenye mamlaka za serikali za mitaa pamoja na sekretarieti za mikoa.”
“Kati ya watumishi hawa 1,164 ambao wanakaimu nafasi bila vibali vya katibu mkuu utumishi, jumla ya watumishi 543 hawana sifa za kukaimu nafasi hizo,” amesema Ndejembi.

Amesema, kwa lengo la kutatua changamoto hii, ofisi hiyo imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kukusanya taarifa za maafisa waandamizi na wakuu 7,008 katika utumishi wa umma wakiwemo watumishi wanaokaimu nafasi hizo ili wafanyiwe upekuzi kwa ajili ya kujaza nafasi za uongozi na zinazokaimiwa kwa muda mrefu.
Naibu waziri huyo amesema, tayari wamekwisha kuanza kufuatilia kujua kwa undani tatizo lilipo huku akionya watumishi kuwakaimisha bila vibali au vigezo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliuliza, “Serikali haioni kuna haja ya kutunga sheria ya mtu kukaimu” muda mrefu ili kuzuia hali hiyo mtu kukaimu zaidi ya miaka miwili.
Akijibu swali hilo, Ndejembi amesema “hili tunalifahamu na tayari tuna kanzidata za watu wenye sifa na sisi tutaendelea kulifanyia kazi ili wenye sifa waweze kukaimu.”
“Nawaagiza watumishi kufikia mwisho wa mwezi huu, kuleta orodha ya watu wanaokaimu bila vibali vya katibu mkuu utumishi na wanaokaimu bila vibali, ili kuona kama wanafaa kuwa hapo tuwaache hapohapo,” amesema Ndejembi.
Vibali vya ukaimu vinafuata upendeleo (hana sifa) au sifa (ana sofa bila uzoefu)?