August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watumia maji pamoja na mifugo

Spread the love

WAKAZI wa Kijiji cha Ndulugumi kilichopo mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma wanalazimika kuchangia maji na mifugo ambayo wanayapata kwenye mabwawa ya kienyeji kutokana na kuharibika kwa kisima cha maji tangu mwaka 2014, anaandika Dany Tibason, Kibaigwa.

Akizungumza kuhusu hali hiyo mkazi wa Kijiji hicho Abdul Mjanja alisema asilimia 90 ya Wananchi wanatumia maji ya kwenye bwawa kwa kunywa na matumizi ya nyumbani   kwa wanachangia na mifugo.

“Wengi hawana uwezo wa kwenda umbali wa km 15 Kibaigwa kununua maji hivyo wanategemea maji hayo ya bwawani kwa kuchangia na mifugo na kwa matumizi ya majumbani ambapo wengine hayatumia maji hayo kwa kuoga hapo hapo bwawani,” amesema.

Amesema kuwa kuna baadhi ya wananchi wenye uwezo wa kununua dawa ya kutibu maji lakini kutokana na hali ngumu wengi wanatumia bila kuyatibu maji hayo ya bwawa.

Aidha amesema wapo akina mama wajawazito wamekuwa wakimeza dawa kwa kutumia maji ya bwawa yaliyochanganywa na dawa hiyo ya kutibu maji hayo jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wake mjumbe wa mamlaka ya mji mdogo Kibaigwa Francisco Liwa alisema kuna haja ya viongozi wa ngazi ya juu ya Kitaifa kufanya ziara kwenye halmashauri hiyo kwa kuwa kuna changamoto nyingi ambazo hawazijui.

Pia aliitaka serikali kuwachimbia visima viwili kama imeshindwa kuwaunganisha na kibawasu(Kibaigwa water supply) ambavyo kwa kiasi kikubwa vitakuwa vimesaidia kupunguza kero ya maji katika Kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyerere Abnel Maige alisema mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira ya mji huo (Kibawasu) imeshindwa kutatua kero ya maji kwa wananchi ikiwemo kutembelea na kubaini maeneo yenye vyanzo vya maji kwa ajili ya kuchimba visima.

error: Content is protected !!