August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watuhumiwa mauaji ya Dk. Mvungi waachiwa

Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Spread the love

SERIKALI imewaachilia huru watuhumiwa wanne kati ya kumi wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kukusudia ya Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, anaandika Faki Sosi.

Watuhumiwa walioachiwa huru ni Ahmad Kitabu (30), Zacharia  Msese (33), Masunga Makenza (40) na  John Mayunga (56).

Pamera Shinyambala, wakili wa serikali amesema kuwa  Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP), hana nia ya kuendelea kuwashtaki watu hao na kwamba amewaondoa katika mashitaka hayo kwa muhibu kifungu cha 91 (1) cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Baada ya taarifa hiyo, Hakimu Thomas Simba ameutaka upande huo kupeleka cheti cha kifo cha mtuhumiwa namba moja ambaye aliripotiwa mahakamani hapo kuwa amefariki. Amesema kuwa kabla ya kufika Mahakama kuu upande huo unatakiwa ufike na cheti hicho ili kuepuka vikwazo.

Watuhumiwa waliobaki katika kesi hiyo ni Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Msungwa Matonya (30) na Longishu Losingo aliyekuwa mlinzi wa Dk Mvungi.

Inadaiwa kuwa, kwa pamoja watu hao walimshambulia kwa mapanga na hatimaye kumsababishia kifo Dk. Mvungi mnamo tarehe 3 Novemba, 2013. Wanadaiwa kufanya kosa hilo la mauaji kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria na Kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

error: Content is protected !!