Tuesday , 27 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Watu wanaishi na wauaji wao
Habari za SiasaTangulizi

Watu wanaishi na wauaji wao

Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
Spread the love

NINAPOKUMBUKA tukio la mauaji ya wananchi walioandamana katika kudai haki ya kuongozwa na kiongozi wanayemtaka, haraka inanijia sura ya mmoja wa watekelezaji wa mauaji hayo, anaandika Jabir Idrissa. 

Alikuwa karibu yangu. Nilimsaidia kufanikisha kazi za kuandika habari na makala. Nilimuamini na kwa kazi aliyokuwa akiifanya ambayo nikiipitia kabla ya kuidhinishwa gazetini, nathubutu kusema “sikuwa na shaka naye kwa chochote.”

Usilolijua ni usiku wa kiza. Nilimjua kwa nje, sio kwa ndani yake. Nilijisahau kwa kumpa imani yote, wakati najua ni kosa kukichukulia kitabu kwa kuangalia gamba lake. Binaadamu tunakosea sana.

Alivyo moyoni mwake katika mtizamo wa kisiasa, ndio sababu ya kumkumbuka kila ninapoingia katika kuyakumbuka mauaji yale ya kikatili dhidi ya wananchi wema.

Huyu alikuja kunitamkia, pengine naye akiamini sitamtizama kwa jicho baya, namna alivyoshiriki kuua wananchi katika siku ya Jumamosi ya Januari 27 mwaka 2001.

Alikuwa mmoja wa askari waliopangwa kushiriki operesheni ya kudhibiti waandamanaji ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Mimi mwenyewe ninaokumbuka kuwaua hawapungui watu saba,” anasema akiniambia katika lugha iliyoonesha anajisikia fakhari kwa kile alichokifanya.

Tamko lake lilinithibitishia mambo mawili: Kwanza, kwamba vikosi maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, navyo vilishiriki mauaji ya wananchi siku ile.

Lakini pili, kwamba uongozi kandamizi wa serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliidhinisha hatua ya ndugu kuwaua ndugu zao kwa bunduki za moto.

Ama ninavyoandika maneno haya, najisikia kuguswa isivyomithilika. Ninayahisi maumivu makali mwilini kama yanayoendelea kuwapata wale waliopoteza wazazi, kaka na dada zao.

Nilishuhudia “mazingira” ya kuuliwa watu wawili wa kwanza katika kadhia ya mauaji ya Januari 26-27 – Imam Juma Khamis wa Msikiti wa Muembetanga na mzee Hamad, aliyekuwa mtumishi wa CCM kwenye Ofisi Kuu za Kisiwandui, Zanzibar – Ijumaa ya Januari 26.

Washuhudiaji waliokuwa wamesali sala ya Ijumaa kwenye msikiti huo, wanasema Imam Juma alipigwa risasi akiwa mlango mkuu wa msikiti, akiwa anatoka nje, mara baada ya dua za baada ya kusali, kumaliza.

“Askari polisi wa FFU walitokea njia ya Mtendeni na mmoja akammiminia risasi Imam Juma pale mlangoni. Nilishtuka sana kwa sababu sikutarajia kushuhudia tukio baya kama lile,” anasema mwanafamilia wa jirani na msikiti ambaye alitangulia kutoka baada ya kusali.

Imam Juma alikuwa kijana bado, na miongoni mwa wale vijana walioshika vizuri ilmu ya dini kiasi cha kuridhiwa na wazee kuwa maimam (viongozi) wa Ijumaa.

Alipigwa risasi wakati askari wakihimiza waumini kutawanyika kutoka msikitini, baada ya kusali, tangazo ambalo lenyewe hata halikutarajiwa.

Msikiti wa Muembetanga, uko ndani ya mtaa mwembamba wenye shughuli nyingi za kiuchumi na pia nyumba za makazi ya wenyeji.

Lilikuwa ni tukio lililoamsha hofu kuu eneo lote la Muembetanga, pamoja na Mtendeni hadi Mchangani ulipo mtaa mrefu wa maduka ya nguo na vitu mbalimbali vingine, ambako watu walianza kukimbizana baada ya kusikia kilichotokea msikitini.

Kutokea Mtendeni yalipo makao makuu ya Civic United Front -Chama cha Wananchi (CUF)- ipo njia nyembamba, au sema “uchochoro” wa kuingilia mtaa wa maduka mengi wa Mchangani.

Ndani ya uchochoro huo ndiko alikopigwa risasi mzee Hamad, ambaye alielezwa na baadhi ya makada wenzake CCM, kuwa alikuwa anaharakia madukani kutafuta bidhaa kabla ya jua kutua.

Ninamkumbuka baba huyu akiishi nyumba mbili-tatu kutoka nilikokuwa nikiishi eneo la Kwahani miaka ya 1980 baada ya kumaliza kidato cha nne. Hawa marehemu wawili, natangulia kuwaombea kwa Mola muumba, amani na msamaha walipokosa.

Siku ya 26 Januari 2001, kama kawaida yangu, nilikuwa mjini Zanzibar. Taarifa za tukio hilo zilinifika nikiwa natoka kusali Ijumaa ile Msikiti wa Jibril kwa Sheikh Ahmad Kizito.

Sikutarajia kusikia mauaji yale kwa sababu sikuiona sababu ya dola kuanza kuua siku hiyo wakati maandamano yalitangazwa kufanyika Januari 27 na nchi nzima, wala sio Zanzibar peke yake.

Kwa muandishi wa habari madhubuti, unajikuta na wajibu kwanza wa kuhangaikia tukio hili kuwa ni habari kubwa gazetini kesho yake. Wakati huo nilikuwa mwajiriwa wa kampuni ya Business Times Ltd (BTL) nikiandikia gazeti la Majira, Dar Leo naBusiness Times la Kiingereza.

Nikashirikiana na waandishi kama mimi kuikamilisha habari. Haikuwa rahisi lakini iliwezekana. Na kweli ilikuwa habari kubwa kwa magazeti ya Jumamosi, Januari 27, siku ambayo maandamano yaliitishwa.

Kwanza ifahamike, uongozi wa CUF uliitisha maandamano nchi nzima kama hatua ya kupinga udhalimu uliofanywa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2000, ambao ulifutwa majimbo 17 ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, kwa sababu nyepesi kama ilivyofanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2015.

Kilichojulikana kwa usahihi kufuatia uchunguzi na rekodi zilizoonekana kabla ya kuharibiwa, ni kuwa wananchi walichagua CUF sio CCM. Ni uchaguzi ambao kwa mara nyingine, ulishangaza wakuu wa CCM kwani katika vituo vingi, vikiwemo vile vilivyotengwa kwa ajili ya askari kupigakura, chama tawala kilikataliwa.

Viongozi wa CUF waliinua sauti kupinga udhalimu wa kufuta uchaguzi wa majimbo 17, lakini hakuna kilichosimamisha mbinu chafu za CCM kung’ang’ania madaraka. Walichokipanga ndicho kilichotendwa.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wakati huo ikiongozwa na Abdulrahman Mwinyijumbe, iliitisha walichokiita “uchaguzi wa marudio wa Novemba 5, 2000,” na kama ilivyotarajiwa, wagombea wote wa CCM, akiwemo wa urais, Amani Abeid Karume, walitangazwa washindi.

Kwa hivyo, tayari kukawa na mgawanyiko katika nchi. Baraza la Wawakilishi likawa na wajumbe wa vyama viwili tu – CCM na CUF – lakini kilicho kibaya kidemokrasia ni kwamba hata kwa Pemba, CCM ilichukua ilipotaka na ikaacha ilipotaka.

Majimbo ya Mkoani, Chambani, Kiwani, Chonga, Pujini na Ziwani, yalitangazwa kuwa yametwaliwa na CCM, kinyume na rekodi zilizokuwa mikononi mwa mawakala wa vyama.

Tume haikufanya ajizi baada ya Novemba 5. Matokeo yalitangazwa haraka, yakimpa Karume ushindi wa asilimia 63 dhidi ya 37 ya Maalim Seif. Aliapishwa haraka vilevile.

Uvurugaji huo wa uchaguzi ndio ukachimba mgogoro kwa mara ya pili, baada ya uliotokea kwa uchaguzi wa 1995, wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa kwa sheria ya bunge, Juni 1992.

Na kwa hakika, hayo ndio mazingira yaliyosukuma CUF kuitisha maandamano nchi nzima. Yalifanyika Dar es Salaam, Geita, Kwimba, Lindi, Mtwara, Mwanza, Bukoba na kwingineko. Lakini yalikuwa dhahiri shahiri Zanzibar ambako hata mauaji ndiko yalikuwa hayafichiki.

Serikali ya Benjamin Mkapa ilipomteua Brigedia Hashim Mbita, akathibitisha angalau watu 31 waliuliwa na vikosi vya serikali.

Hakuna aliyeshitakiwa mpaka sasa. Hata yule niliyekuwa nikimsaidia kazi, hajaulizwa lolote. Ndio kusema, Zanzibar, watu wanaishi na wauaji wao.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Hamahama Ngorongoro kutikisa maandamano ya Chadema Arusha

Spread the loveMAELFU ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na...

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

error: Content is protected !!