TAKRIBANI watu bilioni 1.3 duniani wanakadiriwa kuwa na tatizo la kuona wa namna tofauti. Anaripoti Hamis Mguta … (endelea).
Hayo yameelezwa na Daktari Bingwa wa Macho, Dk. Frank Sandi katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani yanayofanyika kila Alhamisi ya pili ya mwezi wa kumi kila mwaka.
Amesema maadhimisho ya mwaka 2019 yaliyopewa kauli mbiu ya ‘Kuona kwanza’ yana lengo la kuongeza ufahamu kwa watu kuhusu afya ya macho na pia kuwahamasisha wawe na tabia ya kufanya uchunguzi wa macho mapema kabla hayajaathirika zaidi.
Dk. Sandi ambaye ni Rais wa Chama cha Madaktari wa Macho Tanzania, amesema asilimia 89 ya watu wenye upungufu wa kuona wanaishi katika nchi za uchumi wa chini na wa kati, pia asilimia 80 ya ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona wa kati na wa juu unaweza kuepukika.
“Asilimia 55 ya watu wenye upungufu wa kuona wa kati na wa juu ni wanawake na tatizo hili lilikuwa asilimia 4.58 mwaka 1990, tatizo hilo lilipungua na kuwa asilimia 3.37 mwaka 2015,” amesema.
Aidha kwa Tanzania watu wenye tatizo la ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona wanakadiriwa kuwa milioni 1.8 ambayo ni sawa na asilimia 3.37 ya watanzania huku idadi kubwa ya walioathirika na tatizo hilo imetokana na mtoto wa jicho kwa asilimia 39 sawa na watu 695,000, upungufu wa kuona unaorekebishika kwa miwani kwa asilimia 18 sawa na watu 320,000,
Chanzo kingine ni matatizo ya jicho yanayohusiana na umri kwa asilimia 24 sawa na watu 430,000, Shinikizo la Jicho kwa asilimia 10 sawa na watu 180,000, athari ya ugonjwa wa kisukari kwenye pazia la jicho kwa asilimia 4 sawa na watu 71,000, Matatizo ya pazia la jicho kwa asilimia 5 sawa na watu 90,000.
“Tanzania inaungana na mataifa mengine katika kuadhimisha siku hii kwa kutoa elimu ya afya ya macho na kuhamasisha wananchi wote kutumia fursa hii kujitokeza kupima hali ya afya ya macho yao. Shughuli kuu katika maadhimisho ya siku ya afya ya macho kwa Tanzania ni elimu kwa wananchi na upimaji wa afya ya macho kupitia vituo vya tiba vilivyo,” amesema.
Leave a comment