JUMLA ya watu 400 raia wa Misri wamelazwa hospitalini baada ya kung’atwa na nge na kujeruhiwa katika sehemu mbalimbali za miili yao. Pia hadi sasa jumla ya watu watatu wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na wimbi la nge hao ambao wamevamia Mji wa Aswan kusini mwa Misri. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)
Kwa mujibu wa Gavana wa mji huo wa Aswan, Ashraf Attia amesema baadhi ya maeneo watu wamevamiwa na nge baada ya dhoruba za mvua na mchanga kufukua makundi ya nge wenye sumu na kuwashambulia raia.
Kwa kawaida mvua kubwa ikinyesha nchini humo nge husombwa kutoka kweye maficho yao na kuzagaa mtaani kama ilivyo kwa nyoka, ambao pia husombwa na maji kutoka kwenye mashimo yao.
Hospitali na vituo vya matibabu vya Aswan vimejaa wagonjwa walioumwa na nge hao wenye sumu.
Mji wa Aswan kusini mwa Misri ndio ulioathirika zaidi na uvamizi wa nge hao, ambapo mvua kubwa ya mawe pamoja na radi katika eneo karibu na Mto Nile ilishuhudiwa siku ya Ijumaa tarehe 12 Novemba, 2021.
Watu wamehimizwa kupunguza kutembea mitaani na kukaa kwa tahadhari majumbani pamoja na kuepuka maeneo yenye miti mingi.
Aidha, Gavana Attia ametangaza masharti ya watu kutosafiri katika mji huo kutokana na hali ya hewa ya mvua kubwa na ukungu unaosababisha madereva kutoona vizuri.
Mamlaka nchini humo zimechukua hatua ambapo mpaka sasa dozi za ziada za kuzuia sumu zimetolewa kwa vituo vya matibabu katika vijiji vilivyo karibu na milima na jangwa.
Leave a comment