January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watu 28,214 wapata UVIKO-19, 700 wafariki dunia

Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imesema hadi kufikia tarehe 18 Desemba 2021, watu takribani 28,214 wameambukizwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), huku zaidi ya 700 kati yao, wakipoteza maisha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 22 Desemba 2021 na Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, akizindua Mpango wa Serikali wa Harakishi na Shirikishi kwa Jamii Awamu ya Pili, dhidi ya janga hilo, jijini Arusha.

“Takwimu za mwenendo wetu mpaka kufikia tarehe 18 Desemba 2021, jumla watu 28,214 walikuwa wamethibitika kuwa na maambukizi na zaidi ya 700, wamepoteza maisha nchini,” amesema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema, idadi hiyo inaweza ikawa ndogo kutokana kwamba, baadhi ya watu huenda wakawa wameambukizwa na au kufariki dunia kwa ugonjwa huo, bila ya Serikali kupata taarifa zao.

“Hawa ni wale ambao tumeweza pata taarifa zao, tukisema tupate taarifa za kila mtu, hatuna uwezo. Wengine wameugua majumbani, wamefariki hata taarifa hatukupata. Unaweza pata picha kwamba tatizo ni kubwa,” amesema Dk. Gwajima.

Wakati huo huo, Dk. Gwajima amesema kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo, inaongezeka kutokana na visa vinavyoripotiwa kwenye Maabara Kuu ya Taifa na kwamba, ongezeko hilo linasababishwa na baadhi ya wananchi kutofuata taratibu za kujikinga.

“Nchi imeendelea kushuhudia kuongezeka kwa maambukizi mapya ya UVIKO-19, tukiangalia takwimu zetu zimeongezeka, mathalani kama tulikuwa awali tunaona wagonwja wanaoripotiwa kuambukizwa, kupitia maabara yetu kuu ya Taifa labda 14, sasa wamepanda wameshapita mpaka wanafika 47 na kuendelea juu, trend inaongezeka,” amesema Dk. Gwajima.

Waziri huyo wa afya, amewaomba Watanzania kuchukua hatua za kujikinga na kuchanjwa chanjo ya UVIKO-19, ili kupunguza athari zake ikiwemo vifo.

“Chanjo kwa ugonjwa huu faida zake kugeuza mashambulizi yawe mapesi, katika mtu aliyeambukizwa. Ndiyo neema iliyopo badala ya kushambuliwa waende kwenye ugonjwa mkali, ndugu na jamaa kumuunguza waache kwenda kwenye shughuli za maendeleo,” amesema Dk. Gwajima.

error: Content is protected !!