October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Watu 27 mbaroni tuhuma za wizi wa saruji Mbagala

Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam

Spread the love

 

WATU 27 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuiba mifuko ya sarufi, katika ajali ya lori iliyotokea maeneo ya Mbagala, tarehe 5 Oktoba 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 5 Oktoba 2021 na Kamanda wa Jeshi la Polisi la kanda hiyo, Muliro Jumanne Muliro, akizungumza na wanahabari jijini humo.

Kamanda Muliro amesema, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanaiba saruji, katika lori lenye namba za usajili T 705 AUE, lililopata ajali maeneo ya Mbagala, likiwa na mifuko ya saruji 700.

“Polisi walifika mapema eneo la tukio na kuwakuta watu 27, wakiwa wanaiba saruji kwa kuipakia kwenye pikipiki na bajaji. Wote walikamatwa na jumla ya mifuko 368 iliokolewa ikiwemo 10 iliyokutwa kwenye nyumba za watu,” amesema Kamanda Muliro.

Wakati huo huo, Kamanda Muliro amesema, watu wengine 50 wanatuhumiwa kuiba saruji katika lori lililopata ajali jana, maeneo ya Mbagala Mission.

“Mnamo tarehe 04 Oktoba 2021 asubuhi, eneo la Mbagala Mission, lori lenye namba za usajili T 164 DKC aina ya Horse na tela lake namba za usajili T 342 DJZ, likiwa limebeba mifuko ya saruji lilipata ajali na kutumbukia kwenye mtaro, kutokana na tairi kupasuka,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema “baada ya ajali hiyo kutokea zaidi ya watu 50, walijitokeza na kuiba mifuko ya saruji.”

Amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

error: Content is protected !!