Saturday , 22 June 2024
Home Habari Mchanganyiko Watengeneza pombe feki, wakwepa kodi wagunduliwa
Habari Mchanganyiko

Watengeneza pombe feki, wakwepa kodi wagunduliwa

Spread the love

IMEBAINIKA kuwa hadi sasa kuna kampuni 11 ambazo zinadaiwa kujihusisha na utengenezaji pombe kali zisizokuwa na viwango ambazo zimekuwa zikisambazwa sokoni kinyume na sheria. Anaripoti Dany Tibason … (endelea).

Mbali ya kampuni hizo kutokutengeneza pombe ambayo hazina viwango hazilipi kodi kama ambavyo zinapaswa kufanya kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa nyaraka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo mwandishi amefanikiwa kuziona, zimeonyesha kampuni hizo zimelipa sh. 13,566,400 kuanzia Novemba mwaka 2016 na sh. 7,150,000 katika kipindi cha Februari mwaka jana.

Hali hiyo imebainika kutokana na malalamiko kuhusu uwepo wa pombe zisizokuwa na viwango zinazotishia afya za watumiaji na serikali kukosa mapato, imebainika baadhi ya kampuni zinazozalisha pombe hizo hazilipi kodi.

Aidha kampuni mbili zililipa kodi kwa miezi 12 pekee kati ya Januari mwaka 2016 hadi Desemba mwaka jana huku kampuni nyingine ikiwa imelipa kodi katika kipindi cha miezi tisa pekee ndani ya miaka miwili.

Nyaraka hizo zilionyesha kuwa kampuni nyingine iliyoko Mwanza imelipa kodi kwa kipindi cha miezi minne licha ya kufanya shughuli zake kwa miaka miwili.

Pia kampuni nyingine ya pombe kali iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro, ililipa kodi kwa miezi minne kuanzia Januari mwaka 2016 hadi Desemba mwaka jana, kiasi ambacho sawa na kilicholipwa na kampuni nyingie ya vinjwaji hivyo iliyoko Dar es Salaam.

Pia nyaraka hizo zilionyesha uwepo wa kampuni ambayo imelipa kodi kwa mwezi mmoja pekee katika kipindi cha miaka miwili huku nyingine ikilipa kodi kwa miezi saba katika kipindi hicho cha miaka miwili.

Pia zimeonyesha kuwa kampuni nyingine ililipa kodi kwa miezi mitatu pekee huku kampuni moja pekee ya pombe hizo ikiwa imelipa kodi kwa kwa kipindi chote isipokuwa mwezi Aprili na Mei mwaka jana.

Kuibuliwa kwa nyaraka hizo kumekuja wakati ambapo serikali imekuwa ikitoa msisitizo kwa wawekezaji wazawa kuwekeza kwenye viwanda kwa lengo la kutengeneza ajira na mapato ya kodi serikalini.

Akiongoza mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Jumatatu, Rais John Magufuli, alisisitiza umuhimu wa viwanda huku akiwataka wawekezaji kulipa kodi stahiki serikalini.

Hata hivyo licha ya Rais Magufuli, kuwataka wazawa kutumia bidhaa za ndani, bado kuna uwepo wa pombe kali zisizokuwa na viwango.

Mapema mwaka huu wazalishaji wa pombe hizo wakiwemo na wadau mbalimbali wa biashara waliiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya bidhaa hizo zisizokuwa na viwango ili kulinda bidhaa halali sokoni.

Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), kupitia kwa mwenyekiti wao Mkoa wa Dodoma, Deus Nyabiri, alisema serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.

“Si haki kwa wafanyabiashara haramu kuendelea kutawala sokoni. Hii inasababisha ushindani usiokuwa na usawa dhidi ya wafanyabiashara halali ambao wamekuwa wakiunga mkono serikali kwenye uwekezaji wa viwanda,” alisema.

Aliongeza kuwa wawekezaji wanapaswa kuelewa dhamira ya serikali ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda hivyo ni muhimu wakaiunga mkono badala ya kwenda kinyume.

Kwenye Vikao vya Bunge la Februali mwaka huu, baadhi ya wabunge waliitaka serikali kuongeza nguvu kupambana na biashara ya pombe zisizokuwa na viwango kwani zimekuwa zikiuzwa kwa bei nafuu na kuhatarisha afya za watumiaji.

Wakizungumza wakati akichangia hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, walisisitiza pia baadhi ya viwanda vinavyojihusisha na utengenezaji wa pombe hizo havilipi kodi.

“Kwanini serikali inachukua muda mrefu kukabiliana najambo hili linaloathiri viwanda na kusababisha serikali kukosa mapato,” amesema Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde.

Amebainisha kuwa licha ya serikali kuzuia baadhi ya pombe kali lakini pombe hizo zimekuwa zikiingizwa sokoni kwa mtindo mwingine.

Lusinde amesema baadhi ya pombe hizo zimekuwa hazina stika za TBS na TRA na kusababisha kutofahamu ubora wake.

Aliitaka serikali kutoa taarifa kamili ya namna ilivyoweza kukabiliana na sakata hilo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha hoja hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Saddiq, aliitaka serikali kuchukua hatua kali kwa viwanda bandia vinavyotengeneza pombe kali kwa kuwa vimekuwa vikikwepa kodi kwa kuweka stika feki TRA.

Mbunge huyo wa Mvimero (CCM), alishauri kubadilishwa mfumo wa utoaji stika za TRA kwa kuwa zimekuwa zikighushiwa na kusababisha upotevu wa mapato.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Washiriki mbio za NBC Dodoma Marathon kutumia treni ya SGR kwenda Dodoma

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari Mchanganyiko

Upandaji miti uzingatie kuondoa umaskini kwa wananchi

Spread the loveKATIBU Tawala wa mkoa wa Morogoro Dk. Musa Ally Musa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

error: Content is protected !!