January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watanzania walivyoonja machungu ya 2021

Mjane Mama Janeth Magufuli akiaga mwili wa mume wake hayati Dk. John Magufuli

Spread the love

 

MWAKA wa 2021, unaofika tamati leo Ijumaa ya tarehe 31 Desemba, umeacha machungu katika maisha ya Watanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Katika siku 365 za 2021, Watanzania walishuhudia matukio mbalimbali, yaliyowapa machungu, vilio na simanzi, ikiwemo vifo vya viongozi wa kitaifa, mauaji ya kinyama na uhaba wa bidhaa muhimu.

Machungu hayo yalikolezwa moto kufuatia vifo vya viongozi wa kitaifa, akiwemo aliyekuwa Rais John Magufuli, aliyefariki dunia, tarehe 17 Machi  kwa ugonjwa wa moyo, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Kifo hicho kiliacha vilio na simanzi katika mioyo ya Watanzania, kwani hawakuwahi shuhudia kiongozi mkuu wa nchi alyekuwa madarakani akifariki dunia.

Lakini pia, kifo hicho kiliacha msiba mzito famili ya Dennis Mtuwa, iliyopoteza watu watano, katika zoezi la kuuaga mwili wa kiongozi huyo, katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Waliofariki ni aliyekuwa mke wa Mtuwa, watoto wake wawili na wapwa zake wawili.

Rais Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua katika kaburi la Hayari John Magufuli

Walifariki dunia katika mkanyagano wakati wanauaga mwili wa Rais Magufuli.

Mikoba ya Rais Magufuli, ilichukuliwa tarehe 19 Machi na aliyekuwa Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Ikulu ya Dar es Salaam na Jaji wa Mahakama Kuu, Profesa Ibrahim Juma.

Magufuli aliyeingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, aliiongoza Tanzania katika kipindi cha miaka mitano na miezi minne mfululizo, hadi alipopoteza maisha.

Kifo cha Hayati Magufuli kilitokea mwezi mmoja, baada ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, kufariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, tarehe 17 Februari  akipatiwa matibabu ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19).

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Maalim Seif aliyehudumu katika wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kwa takribani miezi miwili (Desemba 2020 hadi Februari 2021), Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Pemba, visiwani humo.

Viongozi wengine waliofariki dunia ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi. Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa.

Mauaji

Miongoni mwa visa vya mauaji vilivyotikisa mwaka 2021, ni mauaji ya Askari Polisi watatu, Miraji Khatib Tsingay, Emmanuel Keralya na Kangae Jackson, na aliyekuwa mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya SGA, Joseph Oktya Mpondo.

Mauaji hayo yalifanywa na Hamza Mohamed, tarehe 25 Agosti, maeneo ya Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.

Hamza aliuawa katika tukio hilo hilo, wakati akijibizana kwa risasi na Askari Polisi, karibu na Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam. Miili ya Aaskari hao pamoja na wa Hamza, ilizikwa katika nyakati tofauti.

Hamza Mohamed, aliyefyatulia risasi Polisi na kuwaua

Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi juu ya uchunguzi wa tukio hilo, zaidi ya kulitaja kuwa ni la kigaidi.

Tukio lingine la mauaji lilitokea tarehe 16 Julai, Mbezi Makabe, wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, baada ya Grace Mushi, kudaiwa kumchoma moto ndani ya nyumba, aliyekuwa mpenzi wake, Khamis Abdallah.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilisema chanzo cha maauaji hayo ni wivu wa mapenzi.

Mauaji wengine yalitokea Desemba, Njiro jijini Arusha, baada ya Patrick Maasi, kudaiwa kumuuawa kinyama mama yake, Ruth Mmasi, ambaye alikuwa mfanyabiashara wa madini. Baada ya kufanya mauaji hayo, inadaiwa aliutupa mwili wa mama yake kwenye chemba ya choo.

Mwili wa Ruthi  ulizkwa jijini Arusha, tarehe 27 Desemba mwaka huu, huku mtuhumiwa wa mauaji yake, akishikiliwa na Jeshi la Polisi.

Kukamatwa kwa Mbowe

Tukio lingine lililoacha simanzi na uchungu kwa baadhi ya Watanzania, hasa wa vyama vya upinzani, ni kukamatwa kwa Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania-Chadema, Freeman Mbowe, lililotokea usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai, jijini Mwanza.

Mbowe alikamatwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, ikiwemo la kupanga kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, ambaye kwa sasa anatumikia adhabu ya kifingo cha miaka 30 gerezani.

Kiongozi huyo wa Chadema, anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi, katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili na wenzake, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo Na. 16/2021 ni waliokuwa Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Mwanasiasa huyo mkongwe katika siasa za upinzani, kwa sasa anashikiliwa mahabusu ya Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam, baada ya kuletwa jijini humo akitokea Mwanza.

Viongozi mbalimbali mashuhuri nchini, wakiwemo wa vyama vya siasa, wa dini na hata wa jumuiya za kimataifa, wametoa wito kwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuifuta kesi hiyo inayosikilizwa mbele ya Jaji Joachim Tiganga, bila masharti.

Tozo ya miamala ya simu

Tozo mpya ya miamala ya simu, ilipitishwa bungeni na kuanza kutumika tarehe 15 Julai, ambapo Serikali ilikuwa inakata kuanzia Sh. 10 hadi 10,000, kuilingana na kiasi cha muamala husika. Fedha hizo zilipangwa kutekeleza miradi mbalimbali, kwa ajili ya kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.

Lakini makundi mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia na wananchi wa kawaida, walipinga tozo hiyo wakidai inaongeza ukali wa maisha kwa wananchi, huku wakipendekeza kiwango cha tozo hiyo kipunguzwe.

Baadhi ya wadau wa watetezi wa haki za binadamu, ikiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), walitinga katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kupinga tozo hiyo, kesi inayoendelea kusikilizwa hadi sasa.

Agosti 2021, Serikali ilitatua makali ya tozo hizo, na kuamua kupunguza viwango vyake kwa asilimia 30

Mgawo wa maji, umeme

Mwaka 2021 ulikuwa mchungu kwa Watanzania, katika baadhi ya mikoa, baada ya kuibuka kwa mgawo wa maji na umeme, ambapo baadhi ya maeneo wakazi wake walikabiliwa na upungufu wa huduma hizo muhimu.

Novemba 2021, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), ilitangaza mgawo wa maji katika mkoa huo na wa Pwani, huku ikitaja sababu kuwa ni, kupungua kwa uzalishaji maji kutoka lita 520 milioni hadi lita 460 milioni kwenye Mto Ruvu.

Kwa upande wa pili, mikoa takribani 11 nchini ilikabiliwa na changamoto ya upungufu wa umeme, kwa saa 12, kutokana na matengenezo yaliyokuwayanafanywa na shirika hilo katika njia ya kusafirishia umeme wa Kilovoti 220 kutoka Kidatu hadi Iringa.

Uhaba wa mafuta ya kupikia ‘Mafuta ya kula’

Mwaka 2021, Watanzania walionja machungu ya uhaba wa mafuta ya kupikia, changamoto iliyopelekea bei ya bidhaa hiyo kupanda.

Sakata la uhaba wa mafuta ya kula, lilianza kutikisa mwishoni mwa mwaka 2020 na kuendelea hadi 2021, ambapo ilipeleka  kupaa kwa bei ya bidhaa hiyo.

Bei ya mafuta ya kula kwa lita 20, ilipanda kutoka Sh. 50,000 hadi kufikia zaidi ya Sh. 80,000. Lita moja ya mafuta hayo ilikuwa inauzwa Sh. 3,000 lakini kwa sasa inakadiriwa kuwa ni Sh. 5,000, huku kipimo kidogo kianza kuuzwa kwa Sh. 500 hadi 700 katika baadhi ya maeneo.

Serikali ya Tanzania, kupitia Waziri wa Uwekezaji, Geofrey Mwambe, ilisema bei hiyo imepaa kutokana na athari zilizosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), zilizopelekea nchi wazalishaji duniani kusuasua kuzalisha na kusafirisha bidhaa hiyo.

Wamachinga

Sakata la wamachinga liliibuka, baada ya Rais Samia kuagiza wakuu wa mikoa kuwapanga wafanyabiashara wadogo katika maeneo rasmi, kufuatia agizo hilo baadhi ya wakuu wa mikoa walianza kulitekeleza kwa kuwaondoa katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo pembezeno mwa barabara.

Hamisha hamisha ya wamachinga ilishika kasi mkoani Dar es Salaam, ambapo baadhi ya wafanyabiashara hao waliilalamikia hatua hiyo wakidai maeneo waliyopelekwa hakuna biashara.

Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma), liliomba kuzungumza na Rais Samia ili wamweleze changamoto zao kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi, wakidai hali zao kiuchumi zimeyumba kutokana na kushindwa kufanya kazi.

Kuungua soko la Kariakoo

Tukio hilo lilitokea usiku wa tarehe 10 Julai, ambapo Rais Samia aliagiza uchunguzi ufanyike ili chanzo cha moto huo uliounguza maduka zaidi ya 400 na kuathiri wafanyabaishara 224, kijulikane. Kufuatia agizo hilo, tume hiyo iliundwa.

Tarehe 27 Julai, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokea taarifa ya matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo, hata hivyo taarifa hizo hazikuwekwa wazi kwa umma. Mwanzoni mwa Desemba mwaka huu, Rais Samia alitoa Sh. 28 bilioni, kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua soko la Kariakoo lililoungua moto jana jioni

Tunakutakia Kheri ya Mwaka Mpya wa 2022

error: Content is protected !!