
Wananchi wakishiriki uchaguzi waviongozi wao
TUNAPOELEKEA katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, Watanzania wanapaswa kujiuliza kama wako tayari kuuza uhuru wao na kununua utumwa kwa kukubali kudanganywa kwa fedha na maneno matamu.
Wako viongozi wabovu ambao wako tayari kununua uongozi kwa gharama yoyote ile ilimradi waendelee kufaidi utamu wa madaraka na fahari zake bila kujali Watanzania wanaumia kiasi gani.
Watnzania wataendelea kuwa watumwa kwa kukosa huduma muhimu za kijamii kama maji safi miaka nenda rudi huku wakilazimika kutembea umbali mrefu na kina mama wajawazito wataendelea kujifungulia sakafuni na vichakani na kura wamepiga. Kama sio utumwa ni nini
Tanzania itaendelea kuwa masikini na omba omba kwa mataifa ya Ulaya licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali za kila aina iliyonao.
Utumwa huu usipoondolewa kwa kupiga kura kwa kiongozi aliye bora, basi utadumishwa kwa kumchagua kiongozi mbovu kwa sababu tu ametoa kitu kidogo au ana maneno matamu ya ushawishi.
Rushwa ni kama kipande kifupi cha nguo kinachositiri sehemu ndogo ya mwili na kuacha sehemu kubwa ya mwili huo ambayo ni nyeti ikiwa wazi.
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa “Mtu yoyote anayenunua madaraka aogopwe kama ukoma.”
Ukitafakari kwa kina na kufanya ufuatiliaji, utagundua kuwa wanasiasa wanaonunua watu tayari wenyewe wamenunuliwa. Sasa watazirudisha vipi hizo fedha kama sio kuuza nchi?
Wanasiasa ni watu wa kuwatafakari sana kabla ya kuwapa uongozi wa nchi. Maana kama wanaweza kutafuta fedha gizani ili kufadhili harakati zao, je baada ya kuingia madarakani, hao waliowaweka wanafanyiwa nini kama si kutii matakwa yao?
Mfumo huu wa nipe nikupe, unazalisha kupe wanaoinyonya damu Tanzania. Kupe hawa wafyonza madini na rasilimali zingine na sasa wanakodolea macho gesi na mafuta.
“Mpaka lini Mtanganyika ataendelea kuwa mdanganyika.” Anaeleza msanii Bonta katika wimbo wake wa Mauwongo unaolenga maudhui ya uchaguzi.
Ni wakati wa Mtanzania kuamka na kuhakikisha kuwa unafanya maamuzi sahihi, kura yako ilete mabadiliko isiwe kiini macho.
Mwandishi wa makala haya ni Ferdinand Shayo, ambaye anapatikana kwa;
ferdinandshayo@gmail.com, 0765938008
More Stories
Uholanzi, Uturuki ‘waingia’ vitani
Kuvunjwa kwa Jiji la Dar giza nene latanda
Ukomo wa urais uheshimiwe