September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watanzania 269 wanahisiwa kuwa na Kifua Kikuu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Spread the love

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa katika kila Watanzania 100,000, kati yao 269 wanahisiwa kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu huku watu 70 wanafariki kila siku kutokana ugonjwa huo ambao ni sawa na watu watatu hufariki kila baada ya saa moja. Anaripoti Hamis Mguta … (endelea). 

Ameyasema hayo leo katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za kifua Kikuu na kutoa tamko kuhusiana na ugonjwa huo katika Hospitali ya Mbagala, Dar es salaam.

Akitoa takwimu za Kifua Kikuu, Waziri Ummy amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa Kifua Kikuu na inakadiriwa kuwa wapo wagonjwa takribani 154,000 ambao huugua ugonjwa wa kifua Kikuu kila mwaka.

“Huduma za matibabu ya Kifua Kikuu (TB) sugu zimesogezwa karibu kwa wananchi, ambapo kwa sasa tunazo hospitali 93 za kutibu Kifua Kikuu sugu ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo, huduma za matibabu zilikuwa zinapatikana katika Hospitali ya Kibong’oto pekee.

“Watu 70 kila siku hufariki kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu, kwa hiyo kila saa moja wagonjwa watatu wanafariki kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu ambao unatibika,” amesema.

Amesema kuwa takribani wagonjwa 154,000 wanaokadiriwa kuugua ugonjwa huo wanapaswa kufikiwa na kuingizwa katika mpango wa matibabu kila mwaka ili kuutokomeza.

“Ifahamike kuwa mgonjwa wa kifua Kikuu ambae hajaanza matibabu anaweza kuambukiza kati ya watu kumi hadi watu 0 kwa mwaka, hivyo tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha tunawafikia wote wanaougua ili tuweze kuzuia maambukizi mapya ya Kifua Kikuu,” amesema.

Mbali na hayo, ameeleza kuwa kitaifa inakadiliwa kuwa wapo wagonjwa wa Kifua Kikuu sugu takribani 200 na kati yao, wagonjwa 167 sawa na 84% walianzishiwa matibabu, huku akitoa wito kwa wagonjwa wengine kujitokeza kupata matibabu.

Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Felix Lyaviva, Mkuu wa Wilaya ya Temeke amemuomba Waziri Ummy kuona ulazima wa kuipanua Hospitali ya Mbagala ili kurahisisha utoaji huduma za Afya, kwani takribani wanawake 67 mpaka 70 hujifungua kwa siku.

“Wakina mama wanaojifungua hapa ni wengi sana, kwa mfano jana tu wakina mama 67 wamejifungua, siku nyingine wanafika 70 mpaka 80, hivyo tunahitaji ipanuliwe hospitali hiyo,” amesema.

Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mbagala, Dk. Dk Ally Mussa amesema kuwa kutokana na maboresho makubwa ya hospitali kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa hadi kufikia wagonjwa 1,700 kwa siku, kumekuwa na maboresho makubwa ya huduma za mama na mtoto, maboresho ya huduma za uchunguzi wa magonjwa (maabara za kisasa).

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa baada ya maboresho mengi katika huduma za Afya za hospitali, kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa hadi kufikia wagonjwa 1,700 kwa siku,” amesema Dk. Mussa.

error: Content is protected !!