Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy, Dk. Jasson Rweikiza ameahidi kutoa simu ya iphone macho matatu kwa mwanafunzi wa kidato cha sita atkayepata daraja la kwanza kwenye mitihani ya kidato cha sita. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki.
Dk. Rweikiza alisema kwa namna wanafunzi hao walivyoandaliwa na kupata matokeo mazuri kwenye mitihani ya majaribio ana matumaini kwamba asilimia kubwa watapata daraja la kwanza.
“Nimeahidi iphone macho matatu lakini kutokana na namna mlivyoandaliwa nimeanza kuwa na wasiwasi nkwamba iwapo wote mtapata Division I nitapata wapi fedha za kuwanunulia iphone nyinyi wote,” alisema
Alisema matokeo mazuri ya shule hiyo yanatokana na mazingira mazuri ya kusomea ikiwemo chakula kizuri, maji ya uhakika na umeme na maktaba za kisasa.

Alisema shule imeendelea kuhakikisha inakuwa na madarasa bora nay a kutosha ili darasa likae na wanafunzi wachache kumwezesha mwalimu kumiliki darasa vizuri ili wanafunzi wamwelewe.
Alisema shule hiyo ina maktaba nzuri iliyosheheni vitabu vingi vya kiada na ziada na mazingira safi ya kusomea kama viyoyozi na huduma ya afya ya uhakika kwa wanafunzi.
Alisema shule imeendelea kujiimarisha zaidi na imeweka uzio eneo lote la shule na ina askari wa kutosha wenye mafunzo na uwezo wa kutumia silaha za moto pamoja na mbwa wakali kwaajili ya ulinzi wa shule.
Alisema kutokana na sababu za kuwepo kwa majanga ya moto kwenye maeneo mbalimbali shule imechukua tahadhari ya kujikinga na ajali zitokanazo na moto kwa kuweka vifaa vya kuzimia moto.
Dk. Rweikiza aliiomba serikali kuwapunguzia kodi wamiliki wa shule ambao alisema wanalipa kodi 18 hali inayofanya kiwango cha ada kuwa juu hivyo kuwabebesha mzigo wazazi.

Alisema iwapo kodi hiyo ingepungua huenda ada nayo ingeshuka hivyo kuwapunguzia mzigo wazazi na kwamba kupungua kwa ada kungesababisha wanafunzi wengi kupata elimu.
“Kodi ni nyingi sana michango Manispaa Kata, kodi za moto na leseni mbalimbali tunaomba ziangaliwe kwa maana ya kumpunguzia mzigo wazazi,” alisema
Dk. Rweikiza alirudia ahadi yake kwamba hakuna mwanafunzi wa shule zake ambaye atafukuzwa shule iwapo atafiwa na wazazi akiwa anasoma kwenye shule hizo.
“Hii ni ahadi yangu ya muda mrefu na narudia tena mwanafunzi yeyote ambaye atafiwa na mzazi akiwa kwenye shule hizi hatafukuzwa shule, awe shule ya awali, msingi au sekondari ataendelea kusoma hadi amalize,” alisema Dk. Rweikiza.

Kwenye hotuba yake, Kamishna wa Elimu, Dk. Mutahabwa aliipongeza shule hiyo kwa namna ambavyo imekuwa ikifanya vizuri kwenye mitihani yake ya kitaifa.
Alimpongeza Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye elimu na kwamba amekuwa msaada mkubwa kwa serikali ya awamu ya sita.
Alielezea kufurahishwa na umahiri ulioonyeshwa na wanafunzi kwenye lugha ya Kiswahili na Kingereza na kuwataka walimu wa shule hiyo wasibweteke na badala yake waendelee kufundisha kwa bidii.
Wakati huo huo, wanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi St Anne Marie Academy wamemshangaza Kamishna wa elimu nchini, Dk. Lyabwene Mutahabwa kwa namna wanavyomudu lugha ya kingereza na kifaransa.
Wanafunzi hao walionyesha umahiri wao wakati wa mahafali ya 15 ya kidato cha sita ambapo mmoja alikuwa akizungumza Kifaransa na mmoja kutafsiri kwa lugha ya Kingereza.
Kamishna huyo alielezea kufurahishwa kwake na umahiri wa wanafunzi hao huku akipongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na shule hiyo jambo ambalo linasaidia jitihada za serikali.
Leave a comment