Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Wataka utafiti kubaini athari rushwa ya ngono kwa wanahabari
Habari Mchanganyiko

Wataka utafiti kubaini athari rushwa ya ngono kwa wanahabari

Spread the love

WADAU wa vyombo vya habari nchini Tanzania wameshauri utafiti ufanyike kuhusu hali ya unyanyasaji wa kingono mahali pa kazi, ili kujua ukubwa wa tatizo hilo na kuweka mikakati ya kuutokomeza. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam… (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatano, tarehe 20 Aprili 2022, jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa wanahabari ulioandaliwa na Shirika linaloshughulikia masuala ya habari, Internews kwa lengo la kujadili sera ya jinsia kwenye vyombo vya habari.

Akiwasilisha mada kuhusu hali ya unyanyasaji wa kingono kwenye vyumba vya habari, Mhariri Mkuu wa Gazeti la Uhuru, Jane Mihanji, amesema utafiti wa kina juu ya suala hilo lazima ufanyike, kwa kuwa ni janga la kitaifa.

“Ni wajibu wetu kueleza ukweli juu ya hili na tutapataje ukweli kama hatuna ushahidi? Inabidi tufanye utafiti. Utafiti wa kina tunapaswa kuufanya, hili ni tatizo la kitaifa, kokote unakoenda  haya matatizo yapo,” amesema Mihanji.

Aidha, Mihanji amewataka wafanyakazi wawe na maadili kwa kuepuka kufanya vitendo vitakavyopelekea wafanyiwe unyanyasaji wa kingono kazini.

Naye Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania, Neville Meena ameshauri sheria na sera zilizotungwa na Serikali kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kingono, zitumike katika vyombo vya habari kwa kuwa vinasaidia kudhibiti vitendo hivyo.

Meena ametoa ushauri huo wakati akiwasilisha mada kuhusu namna sheria na sera zilizotungwa zinavyosaidia katika utokomezaji wa suala hilo.

“Kuwe na utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi, kama kuna malalamiko liitishwe shauri kwa ajili ya kusikiliza mlalamikaji na walalamikiwa pamoja na mashahidi kwa ajili ya kutoa uamuzi. Mwisho wa siku ukifuata utaratibu itasaidia na tuna mahali pa kuanzia sababu sheria zetu zinasaidia,” amesema Meena.

Aidha, Meena ameshauri kila chombo cha habari kiwe na chombo maalumu, kitakachoshughulikia masuala ya unyanyasaji wa kingono mahali pa kazi.

“Kuwe na mifumo inayofanya kazi kwenye vyombo vya habari ambavyo vitatengeneza mifumo ya kampuni itakayoshughulikia unyanyasaji huo,” amesema Meena.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile amesema wanawake wengi wanakosa kazi kutokana na kukataa kutoa rushwa ya ngono.

“Changamoto ya rushwa ya ngono katika ajira ipo, wanawake wengi kwa namna fulani wakati anaomba kazi alikutana na hiyo changamoto kuombwa rushwa ya ngono na hii imekuwa sababu wanawake kukosa kazi,” amesema Tike.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la FHI 360, Andrea Bertone ameelezea utafiti uliofanywa na shirika lake kwenye masuala ya ushirikishwaji mambo ya jinsia, usawa na ulinzi katika jamii, ameshauri mafunzo ya kuwajengea uwezo yatolewe kwa wanahabari hasa wanawake, ili wapate uwezo wa kushindana kazini.

Bertone amesema waandishi habari wanawake wakijengewa uwezo, itapunguza vitendo vya unyanyasaji wa kingono kazini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!