August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watafiti watakiwa kusaka mbegu ya miwa milimani

Shamba la miwa

Spread the love

CLIFFORD Tandari, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro amewataka watafiti wa zao la miwa kuhakikisha wanapata mbegu zinazostahimili kilimo cha milimani ili kuachana na dhana iliyojengeka ya kulima maeneo yenye mabonde pekee, anaandika Christina Haule.

Tandari ameyasema hayo katika kikao cha saba cha wadau wa sukari kilichofanyika mkoani hapa ambapo ameeleza kuwa mbalimbali za nje kama vile Mauritius wanalima miwa juu ya milima na kwamba upatikanaji wa mbegu za miwa ya kulimwa milimani utaboresha uzalishaji wa zao hilo.

“Tusijivunie tani laki 3 tunazopata kwa sasa, tunapaswa kuvuka zaidi. Wenzetu wanazalisha hadi tani laki 8 lakini Tanzania tupo kwenye uzalishaji wa tani laki 3 huku mahitaji yakiwa ni tani laki 4.5, hata watumiaji wa ndani nao wanakosa sukari,” amesema.

Kwa upande wake Dk. Kido Mtunda, ofisa Mfawidhi wa kituo cha utafiti wa miwa Kibaha amesema kuwa, wanaendelea kufanya utafiti ili kuona namna ya kuweza kukidhi mahitaji ya wakulima katika ubora wa mbegu.

Dk. Mtunda alisema, kituo hicho kinaendelea na tafiti mbalimbali ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na pembejeo zilizobora kulingana na maeneo kilimo kinapolimwa huku wakizingatia utoaji wa elimu ya shamba darasa katika maeneo ya Kilombero na kilosa.

“Kituo chetu mpaka sasa kina mbegu bora za miwa zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambazo ni N2 na N41 huku kikiwa na mbegu zinazofaa katika kilimo kwa maeneo yanayohitaji mvua kwa kutumia mbegu aina ya MCO 376,” amesema.

Henry Semwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania akizungumza katika mkutano huop, amewataka wadau wa sukari wakiwemo wenyeviti wa wakulima wa miwa mikoani kushirikiana na watafiti ili kuweza kupata mbegu bora za kuweza kuongeza uzalishaji katika zao hilo.

error: Content is protected !!