January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wataalamu watahadharisha wimbi la nne UVIKO-19, wahimiza chanjo

Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Maelezo

Spread the love

 

WATAALAMU wa sekta ya afya nchini, wameitahadharisha jamii juu ya ujio wa wimbi la nne la Ugonjwa wa Korona (Uviko-19), huku wakihimiza wananchi kuchanja chanjo ya ugonjwa huo kujiupesha na madhara yake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumamosi, tarehe 27 Novemba 2021 katika semina ya wanahabari kuhusu afua za kinga dhidi ya tishio la wimbi la nne la UVIKO-19 na chanjo ya ugonjwa huo.

Semina hiyo iliandaliwa na Wizara ya Afya, ikishirikiana na Shirika linaloshughulika na masuala ya afya, Amref Health Africa Tanzania.

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, amesema wimbi hilo bado halijaingia nchini, lakini Serikali inaendelea kushirikiana na watalaamu wa afya kuangalia namna ya kulidhibiti.

“Kweli wimbi la nne limeripotiwa, kwa sasa Tanzania bado hatujawa na mtu yoyote ana maambukizi ya wimbi la nne, hatuna uthibitisho hata sasa. Lakini majadiliano na viongozi yanaendelea sababu hatuna namna lazima tuchukue hatua,” amesema Msigwa.

Msigwa ametoa wito kwa wananchi kuchanjwa chanjo ya UVIKO-19, ili kujikinga dhidi ya janga hilo.

Meneja wa Programu Mpango wa Taifa wa Chanjo, Dk. Florian Tinuga, amewaomba wananchi wachanjwe chanjo ya UVIKO-19, kwani hadi sasa haijulikani wimbi hilo la nne litakuwa na madhara gani.

“Sasa hivi tunaona wave (wimbi) ya nne inazunguka tu na chanjo ziho zinakuja, tunataka watu wakachanje. Ile wave inayokuja ukali wake hatuwezi kuuona kama tunavyoshuhudia wave zilizopita,” amesema Dk. Tinuga.

Dk. Tinuga amesema hadi kufikia wiki iliyopita zaidi ya Watanzania milioni 1.3 wamepata chanjo hiyo, ikiwemo watumishi wa umma zaidi ya 100,000.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Deodatus Kakoko, amewatoa wasiwasi wananchi kuwa chanjo hizo haina madhara kwani zimechunguzwa na taasisi za Serikali, na kubainika hazina madhara.

Prof. Kakoko ametaja taasisi hizo ikiwemo, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Taasisi ya Taifa ya Utaiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR) na vyuo vikuu kadhaa.

Mkurugenzi wa Ufundi Amref, Rita Mutayoba, amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano ya kudhibiti UVIKO-19, ikiwemo kwa kusaidia shughuli za usambazaji chanjo na utolewaji wa elimu kwa umma.

“Chanjo ilivyoingia Amref hatukubaki nyuma, tuliendeleza juhudi ikiwa pamoja na uhamasishaji, usambazaji chanjo ngazi ya mikoa,” amesema Mutayoba na kuongeza:

“Ambapo tunafanya kazi na kamati za mikoa na halmashauri kutoa elimu kwa watoa huduma za afya namna ya kufanya uelimishaji ngazi ya jamii.”

Hivi karibuni Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, ilipokea msaada wa dozi 500,000 za chanjo ya UVIKO-19, aina ya Sinopharm, kutoka kwa Serikali ya China.

Pia, ilipata chanjo aina ya Johnson and Johnson, dozi 1,058,400 na aina ya Sinopharm dozi 1,065,600 kutoka Shirika la Covax kutoka nchini Marekani.

Kwa mujibu wa Dk. Tinuga, Serikali ya Tanzania imepokea dozi ya chanjo za UVIKO-19, takribani milioni nne, kati 24,000,000 ilizotengewa.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), tangu wimbi la kwanza la UVIKO-19, liibuke mwishoni mwa 2019, watu zaidi ya 250 milioni wameathiriwa na ugonjwa huo, huku zaidi ya 5,000,000 wakifariki dunia.

error: Content is protected !!