October 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wassira: Mwenye harufu ya rushwa hana nafasi Ikulu

WAZIRI Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira akiwa jukwaani

Spread the love

WAZIRI Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, ametangaza rasmi nia ya kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku akionya kuwa Ikulu si mahali pa kumuweka kiongozi mwenye ‘harufu’ ya rushwa na ufisadi. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

“Ninaliongea hili si kwa sababu tu ninataka kuwa Rais, bali ni kwa dhati ya moyo wangu na maslahi ya nchi yetu. Hivyo mnipime. Kumbukeni sijatajwa katika kashfa kama za Escrow, EPA, Richmond na nyingine,” amesema.

Wasira amesema Tanzania ina tatizo kubwa la rushwa linalokwamisha jitihada, mikakati na mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

Kutokana na hali hiyo, Wasira amesema vita dhidi ya rushwa na ufisadi havipaswi kutajwa kama maigizo, bali kuwa na dhamira na utashi wa kwa Rais wa nchi na umma.

Akiwahutubia wafuasi wake Jumapili jijini Mwanza katika ukumbi wa Benki Kuu, Wassira amesema hali ilivyo sasa, Tanzania imekithiri kwa rushwa kuanzia ngazi za chini kwenye jamii hadi taifa, hivyo akiteuliwa na CCM hatimaye kushinda uchaguzi huo, miongoni mwa vipaumbele vyake vitakuwa kuwashughulikia kwa vitendo wala rushwa na mafisadi.

Wassira amesema pamoja na nchi kuwa na sheria zinazopaswa kutumika katika kudhibiti vitendo hivyo, inapaswa kuwa na Rais asiyekuwa na ‘harufu’ ya rushwa.

Amesema kuwa,uadilifu wake umejengwa katika maelekezo na mafundisho aliyoyapata kuanzia utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na `warithi’ wake, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete.

Vipaumbele vyake

Wasira ametaja vipaumbele kadhaa atakavyovisimamia ikiwa atafanikiwa kushinda mchakato na hatimaye kuwa Rais, huku akichanganua namna gani utekelezaji wake utakavyokuwa. Vipaumbele hivyo ni;-

Umoja

Amesema ikiwa atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itaendeleza umoja imara wa Watanzania wa imani, itikadi, rangi na tofauti za aina yoyote, kwa vile ni msingi wa kuleta maendeleo na ustawi wa watu.

Amefafanua kuwa, serikali yake itatetea na kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwaleta pamoja raia wote ili washiriki kujenga uchumi wa nchi na kunufaika na rasilimali zilizopo.

Wasira amesema jamii inakabiliwa na matatizo mengi yanayohitaji mfumo na sera thabiti za jumla katika kufikia utatuzi wake.

Elimu

Wasira amesema serikali ya CCM imefanikiwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kukuza kiwango cha elimu, hivyo jukumu la serikali yake kama akichaguliwa, itakuwa ni kuiboresha sekta hiyo.

Amesema ingawa sekta hiyo inapata kiasi kikubwa cha bajeti ya serikali kuliko nyingine, serikali yake itawekeza katika matumizi ya sayansi ili wahitimu wamudu ushindani wa ajira na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Umaskini

Wassira amesema pamoja takwimu za kuwapo ukuaji wa uchumi, lakini Tanzania inakabiliwa na idadi kubwa ya maskini wanaofikia asilimia 28.2 ya raia zaidi ya milioni 43.

Amesema sehemu kubwa ya watu maskini inapatikana vijijini ambapo shughuli kubwa za uchumi wao ni kilimo cha mazao, uvuvi na ufugaji.

Kwa mujibu wa Wasira, uhalisia huo unasababisha umuhimu wa pekee katika kuwekeza zaidi kwenye sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi ili ziendeshwe kwa mfumo wa kibiashara na kuchochea uboreshaji wa maisha ya Watanzania walio wengi.

Wasira amesema umasikini hasa uliobobea maeneo ya vijijini unasababisha watu kuhamia mijini pasipokuwa na ujuzi na taaluma, hivyo kuibua tatizo la ongezeko la watu wa mijini wanaokabiliana na hali kama hiyo.

Kilimo

Amesema ikiwa atachaguliwa kuwa Rais, serikali yake itawekeza zaidi katika kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara kwa kuleta mapinduzi yatakayowezesha wakulima kutumia nyenzo, teknolojia na mbinu za kisayansi.

Wassira ameongeza kuwa, hakuna jawabu lenye tija kwa kupambana na umaskini nchini ikiwa kilimo kitaachwa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya serikali.

“Haiwezekani tukazungumzia kuboresha kilimo kwa kutumia jembe la mkono. Wakulima lazima watumie nyenzo za kisasa kama trekta, hivyo majembe ya mkono yatapelekwa kwenye majumba ya makumbusho,” amesema.

Kwamba, pamoja na kutumia trekta, kutakuwa na uwezeshwaji wa wakulima katika kutumia sayansi ya kilimo, utafiti kwa huduma za ugani na uboreshaji wa miundombinu.

“Kwa ujumla unapokipuuzia kilimo ni sawa na kusema unawapuuzia watu wa hali ya chini walio wengi nchini,” amesema.

Viwanda na masoko

Wasira alisema ujenzi na kufufua viwanja vya ndani ni miongoni mwa vipambele vyake ikiwa atachaguliwa kuwa Rais, kwa vile sekta hiyo inaongeza thamani ya bidhaa na ajira kwa wananchi.

Amesema kuendelea kuuza nje mazao ghafi kunachangia kuimarisha viwanda na kukuza ajira za nje huku Watanzania wakiwamo wakulima wakiendelea kubaki katika dimbwi la umasikini.

Mifugo

Wassira amesema wafugaji ni sehemu ya jamii muhimu katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo ‘serikali yake’ itajielekeza katika kuwawezesha wazalishe mazao yenye thamani yatakayohimili ubora.

Uzoefu wake

Kuhusu uzoefu wa uongozi, Wassira ametamba kwamba “naifahamu Tanzania, Kwa muda mrefu tangu miaka ya 1970, nimeshirikishwa katika uongozi wa nchi yetu tangu nikiwa na umri wa miaka wa 27.”

Ameongeza kuwa mwaka 1970, kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa mbunge wa Mwibara katika Wilaya ya Bunda. Mwaka 1973, aliteuliwa kuwa waziri mdogo (Juniour Minister), na mwaka 1975, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na katibu wa TANU wa mkoa.

“Mwaka 1982-1985, nilikuwa Afisa mwandamizi mkuu ubalozi wa Tanzania Marekani. 1987-1989, Rais aliniteua kuwa naibu waziri wa serikali za mitaa na mifugo na vyama vya ushirika. 1989-1990, niliteuliwa kuwa waziri wa kilimo, mifugo.

“1990-1991, nimekuwa Mkuu wa mkoa wa Pwani na Katibu wa CCM Mkoa. 2005-2015, NILITEULIWA Waziri wa Maji, Kilimo, Ofisi ya Waziri Mkuu Kilimo tena, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu na hatimae kilimo tena hadi sasa,”ametamba Wassira.

error: Content is protected !!