January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wasomi wamshangaa Kingunge

Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwilu akimnadi Edward Lowassa

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), sio taasisi tena, kimegawanyika, kimeparanganyika na hakiwezi kuongoza tena. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Hali hiyo, imetajwa kudhihirishwa na kitendo cha mwanasiasa mkogwe, mwenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya CCM, Kingunge Ngombale Mwiru kutamka hadharani kuwa “mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ndiye pekee anafaa kuwa Rais.”

Mbali na Kingunge ambaye pia ni mwasisi wa TANU, pia wamo baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao ni wenyeviti wa mikoa na wilaya walijitokeza hadharani kuwaunga mkono watangaza nia akiwemo Hamisi Mgeja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na Mgana Msindani ambayeni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida.

Kauli hiyo imetolewa na wachambuzi mbalimbali wa siasa, wakati wa mahojiano na mtandao wa MwanaHALISI Online.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Dk. Azaveli Lwaitama ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Shirikishi cha Josiah Kibira cha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira amesema “ni viashiria kuwa, CCM kimeondoka kwenye taasisi, kimetekwa nyara.”

“Taasisi inafanya mambo yake kwa vikao. Kila mmoja anapaswa kupeleka maoni yake kwenye chama. Kisha vikao vinafanya maamuzi.

“Kitendo cha Ngombare Mwiru kusema Lowassa ndiye mtu pekee anayefaa kuwa rais, huu ni ushahidi mwingine kwamba anakishinikiza chama kumteua Lowassa,” amesema Lwaitama.

Lwaitama amesema wagombea wanaojinadi kwa vipaumbele vyao, wakati chama kina ilani yake, tayari mgombea huyo ameshapanga hata watu wake atakao waweka serikali kutawala.

“Hii maana yake ni utawala wa mtu fulani kutaka kutumia chama cha CCM, kuingia madarakani afanye mambo yake,” ameeleza Lwaitama.

Aidha, Dk. Ditrik Kajanangoma, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Uandishi wa Habari (IJMC) amesema, hatua hiyo inaonesha CCM hakina utaratibu wa kuendesha mchakato wa kumpata mgombea.

“Kinguge hana tofauti kubwa na marais wastaafu kwa hadhi yake na nafasi yake ndani ya chama na taifa. Ushawishi wake ni mkubwa. Madhara yake kwa wagombea na wanachama wa CCM na taifa, itaonekana amenunuliwa na kuingilia mchakato,” amesema Kajanangoma.

Mbali na kuonekana kama viongozi hao wamenunuliwa, Kajanangoma amesema pia ni kuonesha kuchoshwa na hali ya CCM, hivyo wameona wajitokeze mapema kuweza kumshawishi mtu wanaedhani anafaa.

“Ni mara ya kwanza kushuhudia haya tunayoyaona. Ni muhimu CCM kutumia udhaifu huu, badae waweke muongozo na taratibu ili hali hii isijirudie,” ameeleza Kajanangoma.

Kwa upande wake, Mwalimu wa sayansi ya siasa wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally amesema ni muhimu kufanya udadisi na uchambuzi wa haya yanayojitokeza ndani ya CCM.

“Ni muhimu kuangalia misukomo na misuguano inayopelekea haya tunayoyaona,” amesema Bashiru.

error: Content is protected !!