Spread the love

 

WAKENYA ambao hawatokuwa na cheti cha kupokea chanjo dhidi ya virusi vya Corona hawatoruhusiwa kupokea huduma za serikali ya Kenya ifikapo mwishoni mwa mwezi huu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea). 

Tangazo limekuja kufuatia ongezeko la idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo.

Serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Afya ilisema kuwa yeyote ambaye hana cheti hicho hatoruhusiwa kupata huduma kwenye baa, mikahawa, mikutano mbalimbali, ofisi za serikali, huduma za usafiri na kwenye maduka zilizo na leseni za kazi kutoka serikalini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana tarehe 22 Disemba 2021, Katibu katika Wizara ya Afya, Mercy Mwangangi alisema kanuni hizo ni kuhakikisha kuwa nchi imewachanja watu milioni 10 ifikapo mwisho wa mwezi huu.

“Kama hujachanjwa, hutaruhusiwa kupata huduma za usafiri. Hutaruhusiwa kupanda pikipiki, magari ya umma, gari la maoshi hata ndege. Lazima uonyeshe cheti chako cha chanjo,” akasema Dk. Mwangangi.

Hata hivyo, wale ambao hawajapata chanjo sharti watumie barua inayoeleza sababu za kutopata chanjo hiyo kutoka kwa madaktari walio na leseni.

Ameongeza kuwa vyeti vya chanjo havipaswi kuhifadhiwa nyumbani, kwani vitatumika kama uthibitisho na ushahidi kuwa umechanjwa.

Kila kituo au mratibu wa hafla atahitajika kuteua mtu ambaye atapewa jukumu la kuthibitisha vyeti vya chanjo katika sehemu zote nchini.

Pia wafanyakazi na watoa huduma wote katika kila taasisi lazima wawe wamepata chanjo ndipo waruhusiwe kuingia kazini.

Hata hivyo, Dk. Mwangangi alitupilia mbali kauli kuwa chanjo ni ya lazima.

Alisema kuwa yeyote ambaye anataka kutangamana na jamii, sharti achanjwe.

“Si lazima upate chanjo, ila ukitaka kutangamana na watu mbalimbali nchini, lazima uwe umechanjwa na una cheti chako.”

Wale ambao watahudhuria hafla za harusi, kutembelea mbuga mbalimbali pia watahitajika kuwa na cheti chao cha chanjo.

“Kila mmoja ambaye amechanjwa atapakua cheti chake kwenye tovuti ya Wizara ya Afya. Anaweza kuchapisha cheti hicho au kukipakua na kukitumia ikiwa kwenye simu ya kisasa,” akasema Dk. Mwangangi.

Hadi kufikia tarehe 21 Desemba 2021, jumla ya Wakenya milioni 9.2 walikuwa wamechanjwa.

Hii inaonesha idadi ya watu wazima waliopatiwa dozi zote mbili kufikia asilimia 13.4. Vijana 13,845 walio na umri kati ya 15 na 18 wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo aina ya Pfizer.

Katika sampuli 11,197 za watu waliopimwa, watu 3,328 walibainika kuwa na virusi hivyo.

Kenya imepokea jumla ya dozi milioni 23 huku chanjo zinazotumika sana nchini humo zikiwa AstraZeneca/Covishield, Pfizer, Moderna, Sinopharm na Johnson and Johnson.

Hayo yanajiri wiki moja baada ya kesi kuwasilishwa katika Mahakama Kuu ya kusitisha agizo la Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe kufuatia ombi lililowasilishwa na mfanyabiashara, Enock Aura.

Hata hivyo, wiki iliyopita Jaji Antony Mrima alisema agizo la Kagwe halipaswi kutekelezwa hadi kuamuliwa kwa kesi hiyo.

“Mlalamikaji amewasilisha ushuhuda kwamba wale ambao hawatatoa ushahidi juu ya kupokea chanjo watazuiwa kupata huduma muhimu kutoka kwa idara za serikali,” alisema Jaji Mrima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *