TAMKO la Paul Makonda Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam kuwataka watu mbalimbali wanaotuhumiwa kujihusisha biashara au matumizi ya dawa za kulevya kujisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Kati limeitikiwa na baadhi ya watu hao, anaandika Faki Sosi.
Makonda alitaja majina ya watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya ambao tayari wamekamatwa, wanaotakiwa kukamatwa na kuwekwa rumande kupisha uchunguzi pamoja na wanaotakiwa kufika polisi kwa ajili ya kuhojiwa.
Mapema leo asubuhi, saa 4:35 Babuu wa Kitaa ambaye ni mtangazaji maarufu wa kituo cha Clouds TV alikuwa mtu wa kwanza kufika Kituo cha Polisi cha Kati akiitikia wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa. Babuu aliingia katika eneo hilo akionekana mwenye kujiamini huku akitabasamu wakati waandishi wa habari wakimpiga picha.
Baadaye Khalid Mohamed maarufu kama TID, ambaye ni msanii maarufu wa muziki wa RnB aliwasili kituoni hapo. TID alifika saa 5:07 asubuhi, akiwa amevaa miwani, shati nyeusi na suruali nyeupe.
Hamidu Chambuso maarufu kama ‘Nyandu tozi’ au Dogo Hamidu, msanii wa Hiphop aliingia katika eneo la polisi saa 5:37 asubuhi. Nyandu alizua gumzo baada ya kuingia huku akiwa amevaa kanzu nyeupe na kofia na kuwapita waandishi na wapiga picha bila kumtambua.
Waandishi walishituka na kumtambua baada ya kuingia ndani ya eneo la kituo cha polisi na kuulizia pa kuelekea.

Baadaye Wema Sepetu, msanii wa filamu na miss Tanzania mwaka 2006 aliwasili katika kituo hicho akiwa amejisitiri kwa vazi refu na kujifunika kwa mtandio mweusi kichwani.

Baadhi ya wasanii maarufu ambao mpaka sasa bado hawajafika kituoni na waliagizwa kufanya hivyo na Makonda ni pamoja na Rashid Makwiro (Chid Benz), Heri Samir (Mr. Blue) na Rachel maarufu kama Rachel Kizunguzungu.
MwanaHALISI Online itaendelea kukuletea taarifa za moja kwa moja kutoka Kituo cha Polisi cha Kati.
Leave a comment