December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Washindi Bonge la Mpango wakabidhiwa bodaboda, fedha

Spread the love

BENKI ya NMB Kanda ya Kusini imewazawadia washindi watano kutoka mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi Sh 100,000 kila mmoja ikiwa ni droo ya kwanza ya kampeni Bonge la mpango mchongo wa kusini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Huku pia Chama cha Msingi, (AMCOS) cha Ukombozi kilichopo mkoani Mtwara ambacho kimefanya biashara na benki ya NMB kwa kupitisha fedha za mauzo yake ya korosho katika benki hiyo kimezawadiwa pikipiki moja.

Meneja wa mauzo wa Benki ya NMB kanda ya kusini, Roman Degelewa (kushoto) akimkabidhi dereva wa Bodaboda, Bakari Juma (kulia) pikipiki kama mkopo kutoka Benki ya NMB wakati wa kuchezesha droo ya kwanza ya Bonge la Mpango – Mchongo wa Kusini maalum kwa wateja wa mikoa ya kusini hususan kipindi hiki cha mavuno ya korosho iliyofanyika katika benki ya NMB tawi la Mtwara.

Washindi watano ambao wamepokea fedha taslimu ni, Sadati Chitanda kutoka wilayani Nachingwea Mkoani Lindi, wa pili Abrahman Mohamed kutoka Mtwara.

Mshindi wa tatu ni Omary Ndetelani kutoka Mtwara, wanne ni Edward Lubwaza kutoka Wilayani Nachingwea mkoani Lindi na wa tano ni Ahmad Lilanga kutoka Mtwara.

Meneja wa NMB tawi la Mtwara, Derick Fidelis alisema droo hiyo ni maalum kwa wateja wa mikoa ya kusini hususan kipindi hiki cha mavuno ya korosho na benki imetenga Sh15 milioni na pikipiki tano zitatolewa hadi kufikia Desemba ambapo ndio utakuwa mwisho wa kampeni hiyo.

“Ni matumaini yetu wateja wetu wote wa ukanda huu watazidi kuitumia benki yetu ili wajiongezee fursa ya kujishindania fedha taslimu,” alisema Derick.

Meneja mauzo wa NMB Kanda ya kusini, Roman Degelewa alisema, kampeni ya bonge la mpango mchongo wa kusini ambayo ni mahususi kusaidia mchakato mzima wa zao la korosho miongoni mwa wakulima ilizinduliwa mwezi uliopita.

Lengo la kutoa zawadi ya pikipii ni kusaidia viongozi wa AMCOS na wakulima wenyewe katika kurahisisha shughuli za usafiri kipindi hiki cha mavuno.

Katika droo hiyo, Irene Kawili kutoka bodi ya michezo ya kubahatisha Tanzania alishuhudia droo hiyo na alisema yupo kwa ajili ya kuhakikisha droo hiyo inachezeshwa kwa haki.

Aidha, benki ya NMB Kanda ya Kusini pia imetoa mkopo wa boda boda mbili kwa madereva wa vyombo hivyo Bakari Juma na Abdallah Jafari wa Mtwara huku mwenyekiti wa waendesha boda boda mkoani Mtwara, Omar Mbonde akiishukuru benki ya NMB kwa kuwawezesha.

Aidha, aliwataka waliokaokabidhiwa kuwa makini  kufanya kazi na kurejesha marejesho kwa wakati badala ya kufanya anasa.

error: Content is protected !!