January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wasanii wajitafakari kabla ya kuingia kwenye siasa

Msanii wa filamu, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ akitangaza nia kuwania Ubunge Kinondoni

Spread the love

JOTO la Uchaguzi Mkuu linazidi kupamba moto miongoni mwa wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa, huku idadi kubwa ya wasanii wakionesha nia ya kutaka kuitwa waheshimiwa kuanzia mwishoni mwa Oktoba mwaka huu. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hadi sasa baadhi ya wasanii waliotangaza nia ni Joseph Haule (Profesa Jay), Zuwena Mohamed (Shilole), Wema Sepetu, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, Jacob Stephen (JB), Mrisho Mpoto, Suleiman Msindi ‘Afande Sele’ na wengineo kadhaa, wakitaka kwenda kuungana na wenzao Joseph Mbilinyi wa Chadema pamoja na Vicky Kamata kutoka CCM.

Wasanii wengine ambao wanatarajia kugombea Ubunge, ni Kulwa Kikumba ‘Dude’, Jacob Steven ‘JB’, Anselm Ngaiza ‘Sogg Dogg’, Amri Athuman ‘King Majuto’, Kalama Masoud ‘Kalapina’, Juma Chikoka ‘Chopa’ na Mrisho Mpoto na Ummy Wenceslaus ‘Dokii’

Hakuna mwenye uhakika nini hasa kitatokea katika uchaguzi huo, ingawa uwezekano wa wasanii hao kuleta ushindani na hatimaye kushinda ni mkubwa, hasa ukirejea jinsi Sugu alivyoingia pasipo kutarajiwa na wengi.

Ingawa waigizaji hawa wamekuwa na mambo kadhaa nje ya uwanja, hilo haliwezi kuwa jambo lenye kutia shaka juu ya uwezekano wao wa kushinda.

Wengi wamekuwa wakipiga picha na kuona taswira ya bunge hilo litakalokuwa na wasanii hawa, kwani huenda likaongeza mvuto na kulifanya kuwa moja kati ya mabunge yatakayotazamwa sana na watu, kwa lengo la kuwasikia tu wanachosema, bila kujali kama kitakuwa cha maana au la.

Kwa ambao wamekuwa wakifuatilia vikao vingi vya Bunge katika miaka ya karibuni, wameliona kama lililopoteza mwelekeo ambalo linatumia muda mwingi kwa wabunge kurushiana vijembe bila kujali kama mada iliyo mbele yao ina masilahi gani kwa taifa lao.

Wengi wamekuwa wakikerwa na jinsi wabunge wengine wanavyopoteza muda kuzungumza mambo yasiyo na tija kwa taifa na badala yake kuweka mbele sana itikadi ya vyama vyao, hata kama kinachojadiliwa mbele yao ni kitu muhimu kiasi gani kwa nchi yao.

Kwa staili hiyo ya ubunge, wasanii hawa wana nafasi kubwa ya kushinda kupitia vyama vyao, kwani watu wanaona ni bora kuwaona waigizaji orijino wakiigiza bungeni, kuliko wabunge ambao mara nyingi wanaonekana kuwa wasio na mchango mkubwa kwa taifa.

Hata hivyo, hivi ni kweli wasanii hao wamejipima na kujiona wanatosha kuwania ubunge au ni ile janja ya siku hizi ya kutangaza nia ili kuwatia hofu wengine wanaotaka nafasi hiyo?

Maana taarifa ambazo siyo rasmi, zinasema siku hizi watu wengi hutangaza nia makusudi ili kuwapa presha wabunge kwenye majimbo yao, wakiamini kuwa baadaye watafuatwa na ‘kupozwa’ kitu kidogo, kama ambavyo uvumi huo umewahi kuhusishwa na watu kadhaa hapo nyuma.

Kwa sababu katika hali ya kawaida, ni kwa namna gani baadhi ya wasanii hawa, ambao maisha yao yamejaa utata wataweza kupewa kura na wananchi wanaohitaji watu makini wenye kujua matatizo na suluhisho lake?

Siwadharau, lakini siyo vibaya kuwakumbusha kuwa ubunge siyo kitu rahisi kama kupata uongozi wa Bongo Movie au kuwa muigizaji mkuu katika filamu. Ni zaidi ya kuwaimbisha watu katika majukwaa ya muziki yaliyojaa vijana wengi.

Wanapaswa kujua, ubunge unahitaji mtu mwenye uwezo wa kujenga hoja na anayejua wananchi wanahitaji na si vinginevyo.

Lakini pia nikiangalia kwa makini mimi naona siku hizi bunge limeshuka hadhi hivyo kupelekea kila mtu atamani kuingia maana siku hizi bunge limekuwa viwanja vya burudani na sehemu ya kuuza sura ili mradi mkono unaenda mfukoni.

Mimi sizani kama miaka ya siku hizi wanaogombea ubunge wote wanania ya kwenda kusimama badala ya wananchi…hapana, mimi nadhani wanaenda kutafuta rizki kama wengine ambao wapo tu mwaka mzima unaisha hawajawahi hata kuchangia mada zinazoendelea “wauza sura”.

Nitawaona wananchi waajabu sana endepo watawapitisha wasanii ambao wao wenyewe hawajiheshimu wala kufuata maadili ya nchi yetu.yaani aisee hata wavaa uchi watembea uchi wamezagaa mitandaoni kila siku wanaskendo za ngono leo hii waende bungeni? Kweli?

Je wananchi wa kawaida wanajifunza nini kutoka kwao? Je mnadhani watasimama na kuwafundisha nini wananchi? Mh! Mimi nadhani wanaenda kulipamba bunge. Lakini pia nawaonea huruma wale wabunge vijana wataweza kuvumilia? Au ndo vijembe vitazidi bungeni?

Ni mtazamo wangu, naona siku hizi hata vyama vya siasa vinapoteza mwelekeo haswa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mtanisamehe ila ni mtazamo wangu tu, yaani kwasabu kila mtu anahaki ya kuwa kiongozi basi sasa hata mwendawazimu mnamruhusu kuwa kiongozi? Duh! Kweli CCM imeshuka hadhi. Ngoja tuone endapo wasanii wataingia bungeni ilo bunge litakuwa la aina gani?.

Muda mwingine najiuliza au kwa sababu siku hizi soko la filamu na muziki vimezidi kuporomoka ndo maana wasanii wanahama? Wanataka kujaribu na huku bungeni?.

error: Content is protected !!