January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wasanii wachanga walalama kufunikwa na wakongwe

Msanii wa Vichekezo, James Martin 'Kibuyu Msauzi' akihojiwa na mwandishi wa Mwanahalisionline, Sarafina Lidwino

Spread the love

MSANII wa sanaa ya vichekesho, James Kika ‘Kibuyu Msauzi’ amelalamika kutojulikana katika kazi zake, kutokana na kumshirikisha mkongwe wa tasnia hiyo, Musa Yusuf aka Mkude Simba au Kitale.

Kibuyu wa Sauzi, aliuambia mtandao wa MwanahalisiOnline, kuwa kuwashirikisha wakongwe kwenye kazi zako kuna faida na harasa zake, faida ni kukuinua katika kazi lakini hasara kubwa ni kufunikwa.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 27, amemshirikisha Kitale katika filamu yake ya ‘Chizi karogwa tena’ ambayo kwa sasa inafanya vizuri sokoni.

Kibuyu alisema filamu yake imefanya vizuri sana sokoni lakini hakuna Mtanzania anayejua kuwa ni kazi yake binafsi, wengi wanaitambua kuwa ni movie ya Kitale au Mkude Simba.

“Ninaumia sana kila ninapopita nikisikia watu wanaizungumzia Chizi karogwa tena kama filamu ya Kitale. Hii ni filamu yangu ya kwanza baada ya kusota kwa muda mrefu, nimegharamia kila kitu, ikiwa pamoja na kumlipa gharama za uchezaji Kitale,” alisema Kibuyu Msauzi.

Kibuyu Msauzi anasema pamoja na kukutana na changamoto hizo katika filamu ya Chizi karogwa tena, amemshirikisha tena Kitale katika movie yake nyingine iliyopewa jina la ‘Harusi ya teja’ ambayo inatarajiwa kuwa mtaani hivi karibuni.

Alisema wanalazimika kuwashirikisha wakongwe katika kazi zao kutokana na kulazimishwa kufanya hivyo na wasambazaji wa kazi hizo kwani huwa wanagoma kununua kazi zao mpaka atakapoigiza na msanii mkongwe.

Kibuyu Msauzi amewataka wasanii chipukizi kutokata tamaa katika kazi wanazofanya pamoja na kukutana na changamoto wanazokutana nazo mpaka watakapotimiza malengo yao.

error: Content is protected !!