January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wasaka Urais CCM wafika 42

Kamati Kuu ya CCM itakayokuwa na jukumu la kuwachuja watia nia hao 42 na kumpata mmoja

Spread the love

ZIKIWA zimebaki siku nne kabla ya kufungwa kwa pazia la kuchukua fomu na kurejesha kwa ajili ya kutafuta wadhamini katika harakati za kugombea nafasi ya kuteuliwa kuiwakilisha CCM kwenye Urais Oktoba mwaka huu, Banda Shomoko kada wa chama hicho amefikisha idadi ya wagombea 42. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu Shomoko amesema, hana haja ya kwenda Butiama kupata baraka za kuvaa viatu vya Mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa, viatu vya mwasisi huyo vinamtosha.

Licha ya kuwa amechelewa kuchukua fomu mgombea huyo amesema, ameweka mipango sawa ya kupata wadhamini hivyo hadi Julai Mosi mwaka huu atakuwa amerejesha fomu ikiwa ni pamoja na idadi ya wadhamani inayohitajika.

Kada huyo alijitambulisha mbele ya waandishi wa habari kuwa ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari na mwenye Shahada ya Elimu na Uchumi huku akijinasibu kuwa ‘mimi ni greda.’

Amesema, licha ya Watanzania wengi kuonekana kuwa na mashaka naye lakini ameahidi kuwa tayari kuwatumikia na kwamba, atajitahidi kurejesha fomu kabla ya Julai pili licha ya nchi kutokuwa na miundombinu rafiki.

“Ni kweli miundombinu na muundo wa mikoa yetu haifikiki kwa haraka. Mimi ndio greda Julai Mosi niko hapa nikiwa na wadhamini 450 kwa mikoa 15 kama masharti ya chama yanavyotaka, kwanza hapa ninavyosema naungwa mkono na mikoa isiyo chini ya 10,” amesema Shomoko.

Amesema, endapo akipata ridhaa ya kuwa Rais wa Tanzania serikali yake itahakikisha inasimamia vizuri uchumi kupitia kilimo bora na cha kisasa bila kusahau kufufua viwanda hali itakayosaidia Tanzania na wananchi wake kuondokana na umasikini.

Katika ukusanyaji kodi amesema, katika awamu yake ataweka mwelekeo mzuri wa ukusanyaji kwa kuwa ndio utakaoisaidia nchi kuwa na maendeleo.

“Mimi ni mjasiriamali, nikiwa rais wa nchi hii nitahakikisha mambo mengi ya kimaendeleo yanapatikana. Kumbukeni mimi ni greda, majembe yameshapita sasa ni zamu yangu kuweka mambo sawa.

“Nichi hii inahitaji greda kwenda kutatua wimbi la umasikini na mimi kaulimbiu yangu ni ‘kutokomeza umasikini hapa Tanzania,” amesema.

Amesema, tatizo la ajira limekuwa ni sugu kwa vijana na kwamba, atahakikisha vijana wanawezeshwa huko huko vijiweni walipo, akina mama pia katika vikundi vyao walivyovianzisha.

Akipata ridhaa amesema atahakikisha anapambana na rushwa pia ufisadi kwa viongozi wa umma kwa kuweka usimamizi hasa katika Kamati za Bunge la Tanzania.

error: Content is protected !!