January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wasaka ulwa ndani ya visa Z’bar

Spread the love

ORODHA ya wanasiasa wanaotamani urais wa Zanzibar inaweza kuwa ndefu kuliko ilivyowahi kuwa katika historia ya uchaguzi mkuu chini ya mfumo wa vyama vingi Zanzibar. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Wanasiasa 12 wamejisajili ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwania wadhifa huo, na watano tayari wamefika na kuchukua.

Lakini, wakati orodha ikitajwa, tayari visa vinavyohusiana na uchaguzi huo ambao kura itapigwa Oktoba 25 nchi nzima, vimeanza kwa “maharamia” kumteka mgombea kiti cha ubunge, jimbo jipya la Shaurimoyo mjini Zanzibar, na kumnyang’anya fomu za uteuzi.

Orodha ya wanasiasa wenye nia imetangazwa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Salim Kassim Ali, akisema kila anayefika tume, atapatiwa fomu na atahesabiwa atakapoirudisha kwa wakati.

Miongoni mwa waliofika kuchukua, ni Hamad Rashid Mohamed, mwanasiasa mkongwe aliyehamia Alliance for Democratic Change (ADC) miaka miwili baada ya kufukuzwa Chama cha Wananchi (CUF) alichoshiriki kukianzisha na kutoa mchango kukijenga.

Mtaalamu huyo wa uongozi wa biashara, hakueleza hasa anatarajia kufanya mabadiliko gani katika mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini amesema, “Nikishinda urais nitahakikisha nadumisha na kuendeleza misingi ya Muungano kwa manufaa ya Wazanzibari wa kizazi cha sasa na kijacho.”

  • Nitaanzisha shirika la ndege la Zanzibar ambalo mipango imeanza kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo wataalamu wawili wa Kizanzibari wamepelekwa China kujifunza.
  • Nitasimamia matumizi mazuri ya raslimali ardhi, utaalamu na maliasili zake kujenga uchumi wa Zanzibar… programu endelevu ya kuimarisha kilimo, usafiri wa anga na utalii na kuimarisha viwanda na sekta ya uvuvi.

Wa pili aliyechukua fomu ni Mohamed Masoud Rashid wa Chama cha Umma (CHAUMA) ambaye aliahidi kwamba akibahatika kuchaguliwa, atabadilisha mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili uwe wa kitaifa zaidi kuliko kushirikisha vyama viwili – CCM na CUF.

Pia ameahidi kubadilisha sera na mipango ya kujenga uchumi iwe ya kitaifa badala ya kuhodhiwa na chama cha siasa kinachotoa rais.

Kuhusu Muungano, amesema atarekebisha muundo wake ili kuwa na mfumo wa serikali tatu, kila nchi ikiamua mambo yake bila ya kuingiliwa.

“Haiwezekani kwa muundo wa Muungano wa kondoo 99 kwa mmoja,” alisema akimaanisha kuwa Tanganyika ana kundi kubwa la kondoo kuliko Zanzibar.

Mgombea anayetarajiwa kuvuta umma wa Wazanzibari, Maalim Seif Shariff Hamad, anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi Jumapili na kufuatiwa na mkutano utakaofanyika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani.

Haijajulikana mshindani wake mkuu, Dk. Ali Mohamed Shein, anayewakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM), atachukua lini.

Dk. Shein ambaye ni daktari mtaalamu aliyebobea katika mfumo wa mwenendo wa damu, anatetea kiti alichoshika kutoka Novemba 2010.

Kisa cha kwanza cha hatua iliyopo ya wagombea kujaza fomu za uteuzi za tume, kimemtokezea Abdi Seif Hamad, mgombea ubunge kupitia CUF, ambaye ameripoti Polisi kuwa alitekwa.

Amesema tukio lilitokea Agosti 17, akiwa eneo la ndani ya jimbo analogombea, akitokea ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi mjini Zanzibar kuchukua fomu za uteuzi.

“Ilikuwa wakati natafuta wadhamini nilipojikuta ghafla nimezungukwa na kikundi cha watu wapatao wanane waliojifunika nyuso wakaniteka. walinitisha na kunitaka nisalimishe fomu niwakabidhi,” alisema na kuongeza:

“Namshukuru Mungu hawakunijeruhi wala kunipiga. waliniambia wanachokihitajia ni fomu tu niwapatie.”

Aliandikiwa maelezo yake kituo cha Ng’ambo na kupatiwa namba ya RB/6085/2015. tayari amerejea Tume na kupatiwa fomu mpya.

Akiulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alisema hajapata taarifa yake.

Mkadam ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), alisema, “Watu wangu waliopo doria siku ya mkutano wa Chadema ndio walipata taarifa hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye alitoa taarifa kupitia jukwaani wakati akihutubia wananchi.”

Matukio ya visa yanayoashiria vitisho dhidi ya wafuasi wa upinzani, yanatarajiwa kuibuka tena miezi michache tangu maharamia wanaofuatana na Polisi wa serikali, walipokuwa wakivamia wananchi na kuwajeruhi kwa vipigo vya silaha mbalimbali wakati wa uandikishaji wapigakura.

error: Content is protected !!