July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wasafirishaji binadamu wakamatwa

Spread the love

IDARA ya Uhamiaji Dar es Salaam leo imewatia mbaroni watu wanne kwa makosa mbalimbali ikiwemo biashara ya kusafirisha binadamu na kufanyisha kazi wageni bila kuwa na vibali vya kazi nchini, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, John Msumule, Naibu Kamishina Idara ya Uhamiaji, amesema watu hao wamekamatwa katika Wilaya ya Kinondoni tarehe 10 Februari mwaka huu. Miongoni mwa waliokamatwa ni Deogratius Mwanambilimbi ambaye ni mmliki wa Bendi ya Kalunde.

“Tarehe 10 Februari tuliwakamata watuhumiwa wanne kwa makosa tofauti ikiwemo kujihusisha na biashara ya kusafirisha binadamu, ambapo huwasafirisha wasichana wa Tanzania kwenda kufanya kazi hatarishi Uarabuni,” amesema Msumule.

Amesema, mtuhumiwa wa kwanza ni Abdullah Suleiman Mberwa (37) Mkazi wa Magomeni Mapipa jijini Dar es salaam ambaye anatuhumiwa kujihusisha na biashara ya kusafirisha binadamu na kutoa nyaraka za uongo za wasichana wawili ili kuwapatia hati za kusafiria za Tanzania.

“Asma Mkenyenge (26) Mkazi wa Tandika na Nyamizi Kambuga (31) Mkazi wa Mbagala walirubuniwa na mtuhumiwa Abdullah kwenda Uarabuni na kuwataka kufanya siri bila ya kuhusisha ndugu zao. Pia aliwapa masharti ambayo yanaonesha kuwa alitaka waende kufanya kazi ya ngono,” amesema.

Akisimulia jinsi ilivyokuwa Kambuga amesema, walipewa sharti la kuondoka kwa siri, kupima afya hasa Ukimwi, figo na moyo pia waliambiwa wasikutane kimwili na mwanamme yeyote hadi watakapo safiri.

Mtuhumiwa wa pili ni Deogratius Mwanambilimbi (43) Mkazi wa Goba Kinondoni ambaye ndio miliki wa bendi ya Kalunde, yeye anatuhumiwa kuwafanyisha kazi wageni katika bendi yake huku akijua hawana vibali vya kazi na ukaazi.

“Deogratius Mwanambilimbi mwenye mkataba wa kutumbuiza katika Hotel ya Girrafe ana kosa la kuwafanyisha kazi raia wawili wasio na vibali kutoka Kongo DRC ambao ni Kashama Alan Mulumba  na Mwenabantu Kibyabya Michel,” amesema Msumule.

Msumule amesema Wilaya ya Kinondoni inawahamiaji haramu wengi ikilinganishwa na sehemu nyingine nchini na kwamba wataendeleza operesheni wilayani humo.

Tangu operesheni ya kukamata wahamiaji haramu nchini kuanza tarehe 31 Januari mwaka huu, idara imeeleza kukamata wahamiaji haramu 162 baadhi yao wakiwa tayari wamerudishwa kwao huku wengine wakifunguliwa mashitaka.

error: Content is protected !!