January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Warioba, Polepole, Baregu waipopoa CCM

Jaji Mstaafu, Joseph Warioba

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kujivua mapenzi yake kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kutenda haki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Mbali na Kikwete kutakiwa kujivua mapenzi kwa chama chake pia, CCM imetakiwa kutopitisha watangaza nia wenye doa (kashfa mbalimbali) ili kulinda maslahi mapana ya taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na jopo la watoa mada katika kongamano la kujadili “Amani na umoja kuelekea uchaguzi mkuu” lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Akizungumza katika kongamano hilo Humphrey Polepole, aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amesema kama CCM itapitisha wagombea urais wenye doa, wakaachwa kufanya michezo kama walivyofanya michezo katika suala la katiba. Atahamasisha wananchi kutopigia kura CCM.

“Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kusema CCM ikataliwe. Nitasema bila hofu…Watanzania eeeeh… naomba muwanyime CCM Kura zenu. Haya mambo ya kufanya michezo na maendeleo sipo tayari kuyaona.

Mbali na kuikemea CCM, Polepole ameutaka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuacha ubinafsi kwa kuwa kufanya hivyo ni kubomoa misingi ya demokrasia.

Katika kongamnao hilo, Jaji Kiongozi Mstaafu Amir Ramadhan Maneto amesema, “Haki ndio inazaa amani.”

“Tunataka haki itendeke bila ubaguzi wowote. Ndipo amani itakuwepo. Hivyo kuelekea uchaguzi mkuu, Rais Kikwete ajitoe kwenye chama chake. Haki itatendeka,” amesema Maneto ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu.

Amesema viashiria vinaonesha serikali ndio chanzo cha kuvunjika kwa mani hasa katika kipindi cha uchaguzi.

Maneto amelishutumu Jeshi la Polisi, kitengo cha Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kutumika kuanzisha fujo katika maeneo kadhaa ikiwemo mauaji ya David Mwangosi, aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten katika kijiji cha Nyololo mkoano Iringa mwaka 2012.

Profesa Mwesiga Baregu, ambaye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amesema,”…kama uchaguzi hautoonekana kuendeshwa kwa haki. Na matokeo yake sio ya haki, tutakuwa tunavunja amani.”

“Tunaingia kwenye uchaguzi tukiwa na obwe la Katiba. Tulikubaliana kabla ya uchaguzi mkuu ni lazima tuwe na: tume huru ya uchaguzi; mgombea huru; uwezo wa kuhoji matokeo ya rais na rais achaguliwe kwa kura zaidi ya asilimia 50. Yote hayo hatuna. Viashiria vyote vinafanana na yaliyotokea Kenya mwaka 2007 na 2008,” amesema Baregu.

Jaji Joseph Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amesema, “…waasisi wa taifa hili walitanguliza utu, haki na usawa. Walisimamia misingi hiyo. Wagombea 38 ni wengi. Kila mmoja ametoa ahadi. Hawatumii Ilani ya chama. Wengine tunajiuliza ni wagombea binafsi?.”

“Wale ambao wataenda kuwapima wagombea tayari wamejitokeza kuwaunga baadhi ya wagombea. Wao ndio wanaenda kuamua. Je watatenda haki?,” amehoji Warioba.

Pia, Awadhi Ali Said, aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ameeleza kuwa kila mara uchaguzi mkuu katika nchi za Afrika huacha makovu ya machafuko au kutokuwepo kwa maridhiano.

“Ni muhimu kuhoji, muungano wetu wa miaka 50 una amani?, una umoja?, una utulivu?. Unapogusia afya yake ni kama unaunyanyapaa kama vile ni jambo ambalo hatutakiwi tulifanye,” amesema Said.

error: Content is protected !!