Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Warioba aponda uchaguzi mkuu Tanzania, Pinda awapa ujumbe CCM
Habari za SiasaTangulizi

Warioba aponda uchaguzi mkuu Tanzania, Pinda awapa ujumbe CCM

Jaji,Joseph Warioba Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Spread the love

 

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba, ameuponda uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akisema, yalitokea matatizo makubwa ambayo hawajawahi kushuhudiwa na wananchi tangu mwaka 1958 na 1961. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza katika mkutano maalum uliojadili “hali ya demokrasia nchini,” Jaji Warioba alisema, haelewi ni kwanini suala la Tume Huru ya Uchaguzi, limekuwa linaibua malumbano kila baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Alisema, “mimi sijui kwanini tunalumbana, kila baada ya uchaguzi. Ni kawaida yetu kuona udhaifu upo wapi, kisha tunafanya maboresho. Ukiangalia hata sheria ya uchaguzi imefaninyiwa maboresho mengi, yote hayo ni kujaribu kuondoa udhaifu uliopo katika uchaguzi.”

Aliongeza, “lakini kipindi hiki kumetokea matatizo makubwa sana, kwa mara ya kwanza watu wengi wameenguliwa. Hawa Watanzania wamezoea uchaguzi tangu mwaka 1958 na 1961, yanakuja kutokea vitu vingine, ni lazima kuna tatizo, lazima itazamwe, lazima irekebishwe.”

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na waziri mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema, wakati umefika kwa chama chake kukubaliana na upinzani, ili kuanza mchakato wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Vigogo hao wastasafu walitoa maoni hayo, wakati wakizungumza katika mkutano huo wa siku tatu ulioanza tarehe 15-17 Desemba 2021, jijini Dodoma, ambao uliitishwa na Baraza la Vyama vya Siasa na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan. Ulifungwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu

Jaji Warioba aliibua hoja hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu tarehe 28 Oktoba 2020 na kushuhudiwa malalamiko lukuki kutoka kwa vyama vya siasa hususan upinzani.

Akizungumzia suala la mikutano ya hadhara, Jaji Warioba alisema kwa kifupi, suala la mikutano ya hadhara rais ametoa muelekeo, hivyo wakizungumza vizuri wataenda pamoja.

Kauli ya Jaji Warioba iliungwa mkono na waziri mkuu mstaafu, Pinda alisema, “kuna mambo ambayo sisi CCM kama chama tawala, lazima tubebe dhima. Tutoe uongozi.

“Kwa mfano, hili la Tume Huru ya Uchaguzi, kizuizi ni nini? Hili ni jambo ambalo lazima tukubaliane na wenzetu wa upinzani na tuanze mchakato wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi,” alisisitiza.

Kauli za mawaziri wakuu hao wastaafu zimetolewa, wakati vyama vya upinzani vikiwa vinaitaka Serikali kuhakikisha inapatikana Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao, pamoja na kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba mpya.

Kauli ya vigogo hao inaungana na yale yaliyomo kwenye kitabu kilichaondikwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alichokipa jina la “My Life, My Purpose” (Maisha Yangu, Kusudio Langu).

Katika kitabu hicho, Mkapa aliweka bayana kuwa wakati umefika wa kuwepo Tume Huru ya Uchaguzi, ili kumaliza malalamiko ya muda mrefu.

Katika uchaguzi huo ambao Jaji Warioba anasema, ulisheheni dosari nyingi, katika maeneo mengi CCM walitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwa washindi kwa zaidi ya asilimia 90 kwenye nafasi za ubunge na udiwani.

Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage

Mathalani, chama kikuu cha upinzani cha Chadema, kiliibuka na ushindi kwenye jimbo moja pekee – Nkasi Kaskazini, ambako mgombea wake, Aida Kenan alitangazwa mshindi, huku kikipoteza majimbo yake zaidi ya 20.

Hatua hiyo ilitokana na ama wagombea wa upinzani kuenguliwa mapema kwa sababu mbalimbali zilizotajwa na NEC ikiwemo kukosea kuandika herufu za majina yao, vyama vyao lakini pia kudaiwa kushindwa.

Maelfu ya mawakala wa upinzani walienguliwa siku ya uchaguzi, huku wengine wakizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.

Ni katika uchaguzi huo, kulishuhudiwa video zikisambaa mitandaoni zikionyesha jinsi udanganyifu ulivyotawala uchaguzi huo. Hayo yaliripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kigoma. Hata hivyo, NEC ilizikana kura hizo.

Katiba mpya

Akizungumzia suala la Katiba Mpya, Jaji Warioba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema, mchakato wa Katiba unaweza kuendelea ulipofikia kwa kuwa ulizingatia sheria na kwamba hakuna haja ya kuanza upya.

Alisema, “Katiba mpya mchakato wake umezingatia sheria, hivyo hakuna haja ya kusema tuanze upya, pale tulipofikia tunaweza kusahihisha ili tuendelee mbele.”

Safari ya mchakato wa kutafuta Katiba Mpya ulianza nchini mwaka 2010, baada ya Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete kuutangazia umma dhamira na nia ya serikali ya kuanzisha mchakato huo.

Mwaka 2011 kulitungwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Tume ilifanya kazi yake ya kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasmi ya Kwanza na ya Pili, kisha ikaiwasilisha kwenye Bunge Maalum la Katiba, ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa na wajumbe wa kuteuliwa na Rais. Wajumbe wengine walikuwa wabunge wa Bunge la Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Bunge hilo lilioanza pamoja, lilipasuka katikati ya safari, kufuatia wajumbe kutoka vyama vya upinzani na wachache wa kuteuliwa na Rais, kujiondoa bungeni, kwa madai ya kutokukubaliana na mwenendo wa Bunge hilo, ambalo lilikuwa chini ya Samwel Sitta na Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, Bunge hilo liliendelea na kupatikana kwa Katiba Pendekezwa ambayo ilikuwa ipigiwe kura ya maoni mwaka 2015, lakini zoezi hilo lilikwama kutokana na kile kinachoaminika, “kutopatikana mwafaka wa kitaifa.”

Maazimio 80 yafikiwa

Katika mkutano huo wa siku tatu, wajumbe wamekubaliana mambo 80 yanayopaswa kufanyiwa kazi ikiwemo suala la Katiba Mpya, mikutano ya hadhara na utendaji wa jeshi la polisi.

Kwa mujibu wa makubaliano yao, jukumu la kufuatilia na kuhakikisha maazimio hayo yanatekelezwa, yameachwa kwa msajili wa vyama vya siasa, ambaye ataunda kikosi kazi na kutoa mapendekezo kwa baraza la vyama vya siasa.

Baada ya kupokea mapendekezo hayo, Baraza hilo, litayapitisha na kuyapa uhalali, kabla ya kuyafikisha kwa mamlaka husika.

Akisoma baadhi ya maazimio ya mkutano huo kabla ya kufungwa na Rais Mwinyi, Mwenyekiti wa mkutano huo, Prof. Rwekaza Mukandala alisema, wajumbe wameazimia badala ya kuendelea na mchakato wa katiba mpya, wanaweza kuchagua mambo machache yanayolalamikiwa sana na kuanza kuyafanyia kazi.

Pia, kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha sheria ya vyama vya siasa, vyama vya siasa ni haki yao kufanya mikutano ya kisiasa chamsingi kuwepo kwa utaratibu wa kuadhibiana pale au kwa vile ambavyo vinakiuka taratibu hizo.

Prof. Mukundala alisema, suala la mikutano ya hadhara, lishughulikiwe kwani hakuna haja ya kurudi mwanzo bali kinachotakiwa ni kurekebisha sheria ya katiba iliyopo sasa, katiba pendekezwa na kuipitisha.

Kuhusu tume huru ya uchaguzi, Prof. Mukandala alisema yamepokelewa na yanayohitaji kufanyiwa kazi, yatafanyiwa kazi.

“Wanakongamano wameazimia kwamba mkutano kama huu ni muhimu, kwa kuwa unasaidia kudumisha umoja wetu na kutatua changamoto kwa njia ya mazungumzo,” alieleza.

Alisema, “kuna umuhimu wa wadau wa siasa kufuata katiba, sheria, kanuni na miongozo katika kutekeleza majukumu yao. Pia vyombo vyenye maamuzi vina wajibu wa kutenda haki na kulinda amani kwani amani msingi wake ni haki.

“Kwamba vyama vya siasa vitoe nafasi maalumu kwa makundi maalumu husuani wanawake na wenye ulemamvu, kwani michango yao ni muhumu kwa taifa na demokrasia yake inategemea na mazingira ya nchi husika, uchumi, mila, utamaduni na desturi; hivyo tusiwe watu wa kuiga demokrasia ya nchi nyingine.

“Kwamba elimu ya uraia iwe endelevu, ianzie ngazi ya chekecheke isisubiri wakati wa uchaguzi na serikali na vyombo vya dola, viepuke upendeleo vinapohudumia vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla.”

Aliongeza: “Sheria ya vyama vya siasa ifanyiwe mapitio upya na mchakato uwe shirikishi. Nayo sheria ya jeshi la polisi ifanyiwe marekebisho yatakayolizuia jeshi hilo kuwa na visingizio vya kutekeleza sheria.

“Viongozi wa siasa wawe hofu ya Mungu katika utendaji wa kazi zao kuwa waadilifu, watii sheria, wawe na uzalendo na kuwa na uchungu na nchi na kila moja ana jukumu la kulinda amani na utulivu ndani ya nchi na kwamba kila mmoja anatembea katika jahazi moja.

“Manung’uniko na malalamiko ya wananchi na wadau yashughulikiwe mapema. Baraza la vyama vya kisiasa lipewe jukumu la kushughulikia migogoro ndani ya vyama vya siasa.

“Kama kuna malalamiko na kutoaminiana kwa wale wanaotuongoza hasa wale wanaoongoza tume zetu za uchaguzi, hata wakichaguliwa watu wengine, watu ndio sisi Watanzania, hivyo tusipoaminiana maneno yataendelea kwa hiyo kuna haja ya kuongeza kuaminiana, wananchi, vyombo mbalimbali na viongozi wote.”

Akifunga mkutano huo Rais Mwinyi alisema, serikali zote mbili zitayafanyia kazi mapendekezo hayo yaliyopitishwa na mkutano huo kwa masilahi mapana ya taifa.

Aliwasisitiza viongozi hao wa kisiasa pamoja na wadau wa siasa kuitunza na kudumisha amani kwani hata tafiti zinaonesha kuwa Tanzani ni miongoni mwa mataifa saba yenye kiwango kikubwa cha usalama na amani Barani Afrika.

Alisema, Baraza la Vyama vya Siasa lililoandaa mkutano huo, limetokana na miafaka mitatu iliyofanyika kwa nyakati tofauti Visiwani Zanzibar.

1 Comment

  • Asanteni kwa kuwa wakweli. Natumai na viongozi wengine wa CCM watakuwa wakweli nao. Tuache unafiki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

error: Content is protected !!