November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Waraka wa Maulid waibua mauaji haya

Spread the love

WARAKA wa Maulid (Sikukuu ya Maulid) uliotolewa na Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania umeibuka na matukio mbalimbali yaliyotokea nchini. Anaripoti Yusuph Katimba … (endelea).

Waraka huo umetolewa leo Jumanne terehe 20 Novemba mwaka huu ukihoji matokeo ya uchunguzi ya mauaji hayo.

Sikukuu ya Maulid hufanyika kila mwaka kitaifa ambapo Waislam kote duniani huadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W).

Katika waraka huo uliosainiwa na Sheikh Ponda Issa Ponda, katibu wa jumuiya hiyo na kubeba kauli mbiu ‘Haki Ndio Nguzo ya Amani’ umeeleza umuhimu wa usawa na haki za raia kwamba ndio nguzo ya amani.

Waraka huo amependekeza umma uelezwe matokeo ya ripoti mbalimbali za mauaji yaliyotokea nchini na kiini chake.

“Watu huchukuliwa na vikosi vinavyotumia magari aina ya Land Cruser na silaha sawa na zile za serikali.

“Vikosi hivyo hufanya kazi hiyo bila ya hofu wala kuhojiwa na yoyote,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Waraka huo umeeleza kushangazwa na matukio ya watu kutoweka na zaidi mamlaka za dola kushindwa kuieleza jamii kutoweka kwa watu hao na sababu za kutopatikana kwao.

“Katika hali hiyo ya kukithiri viashiria vya kutoweka kwa amani, mwaka huu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipewa taarifa ya mauwaji mengine yaliyofanywa wilayani Kilwa Mkoani Lindi, tena Msikitini.”

Waraka huo umedai kuwa” Msikiti wa Ali Mchumo ulioko Kilwa ulishambuliwa na kuua pia kuteka masheikh zaidi ya kumi waliokuwa ndani ya msikiti huo na kwamba, licha ya Serikali kuahidi kupeleka majibu, haikufanya hivyo.

Umekumbushia yaliyotoke Mei 14, 2017 ambapo vikosi vya serikali vilimuuwa hadharani Imamu wa Msikiti wa Al-Kheri, wa Jijimi Dar es salaam Sheikh Salum Almasi.

“Jeshi la polisi lilidai Imamu Salum Almasi ambaye alikua mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM, alikuwa anataka kuwapora fedha walizokuwa wanaziweka katika mashine ya ATM, madai ambayo hayakuwahi kuthibitishwa.

“Jeshi la polisi pia linalaumiwa katika mauwaji mengine ya Mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji nchini, NIT Akwilina Akwilini Bafta, mauaji yaliyofanyika hadharani.

“Jeshi hilo lilisema risasi walizorusha zililenga hewani zikiwakusudia waandamanaji waliokuwa wanavunja sheria.”

Pia umehoji mauaji yaliyotokea wilayani Tarime, mkoani Mara kwa kuuwa kwa kumchoma kisu Suguta Marwa Suguta aliyekuwa mikononi mwa vyombo vya dola.

“Katika utamaduni huo Oktoba mwaka huu peke yake, imeripotiwa jeshi la polisi kuwauwa wananchi kadhaa wilayani Uvinza mkoani Kigoma katika Kijiji cha Mpeta.

“Katika operesheni hiyo (ya kuwaondoa wananchi katika ardhi inayotakiwa na serikali), jeshi la polisi limedai kupoteza askari wake wawili na wao kuwauwa raia wawili,” umeeleza waraka huo.

Waraka huo umeeleza, mbali na taarifa hizo za kipolisi, taarifa nzito za mauwaji hayo zimeendelea kupatikana.

Na kwamba, mbunge wa eneo hilo, Hasna Mwilima alisema katika mauwaji hayo, jeshi hilo limewaua raia wengi zaidi ya 17 ambapo idadi iliyotolewa na Zitto kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini ni kubwa zaidi.

“Kwa kifupi taarifa za mauwaji ni nyingi sana, na vyombo vya dola vikijitokeza kuhusika na sehemu kubwa ya mauwaji hayo,” umeeleza waraka huo.

Waraka umehoji matokeo ya utekwaji wa watu wakiwemo mashuhuri kuongezeka.

“Kijana Ben Saanane, Sheikh Khatib Yunus, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye, Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, Azori Gwanda na wengine wengi wametekwa na hawajulikani walipo,” unaeleza waraka huo.

Pia umeeleza kwamba, maimamu wengi wa Misikiti na Waalimu wa Madrasa wametekwa na watu wanaotumia magari ya Land Cruser na hawajulikani walipo.

Na kwamba, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa za familia nyingi zinazowatafuta ndugu zao waliotekwa.

Utekaji wa hivi karibuni wa mfanyabiashara maarufu barani Afrika, Mohammed Dewj (MO) umeongeza hofu zaidi nchini.

Waraka huo umeshauri kuwa, sheria za nchi zitazame upya sheria ya kupambana na ugaidi kwa kuww, awali hakukuwa na mauaji ama kupotezwa watu kwa kiwango cha sasa.

“Katika yale mauwaji na utekaji wenye utata serikali ikubali ushauri wa kuunda Tume huru ya uchunguzi. Tume ishirikishe mabingwa wa uchunguzi wa ndani na nje ya nchi.

“Katika matukio yanayogusa Dini na sekta muhimu kama uchumi, uchunguzi wa kina ufanyike kabla na watu wake wanapokamatwa shauri lianze kusikilizwa na kukamilika ndani ya muda unaolinda haki za kisheria,” umeeleza waraka huo.

Sehemu ya waraka huo imeonesha wasiwasi wa kuendelea kuimarishwa amani nchini kutokana na kuwepo kwa matukio ya kuogofya.

Waraka huo umeshauri jamii kuenzi maisha ya Mtume Muhammad (S A.W) kwa kuwa alichukia dhuluma, uonevu, rushwa na udikteta.

“Toka akiwa mdogo Mtume Muhammad alikerwa sana na kuenea kwa maovu na utawala wa dhulma.

“Ulimwengu wakati huo kama ilivyo sasa, ulikuwa umetawaliwa na maisha ya kiholela, dhulma, umaskini, mauwaji, udikteta na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.”

error: Content is protected !!